Tanesco yafanya ukaguzi wa Mita kitaalamu kubaini ukweli malalamiko ya umeme kuisha haraka yagundua mita zipo sawa

📌 Ni kufuatia malalamiko ya baadhi ya wateja kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari

📌 Chanzo cha tatizo kwa mita zilizokaguliwa chatajwa kuwa ni uchakavu wa wiring za ndani ya nyumba na tabia holela za matumizi ya umeme

📌 Shirika kuongeza kasi ya utoaji wa elimu ya matumizi bora ya umeme kwa wananchi

Na Mwandishi Wetu

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limefanya ukaguzi wa kitaalamu wa mita za umeme kwa baadhi ya wateja waliowasilisha malalamiko hayo kwa njia za mitandao katika maeneo ya Tabata Kimanga na Kimara Suka jijini Dar es Salaam.

Malalamiko hayo yaliibuliwa na baadhi ya wananchi mitandaoni na kwenye vyombo vya habari kuhusu madai ya umeme kuisha haraka bila sababu ya msingi.

Zoezi hilo lilifanyika Januari 27, 2026, likiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Irene Gowelle, akiambatana na timu ya wataalamu wa Shirika, kwa lengo la kubaini chanzo halisi cha changamoto hiyo na kujiridhisha kuhusu ufanisi wa utendaji wa mita za wateja.

Matokeo ya Ukaguzi

Baada ya kufanyiwa vipimo vya kitaalamu, TANESCO imebaini kuwa mita zote zilizokaguliwa zilikuwa salama na zinafanya kazi kwa usahihi, kinyume na madai yaliyokuwa yakitolewa kuwa mita hizo zina kasoro ya kiutendaji.

Hata hivyo, ukaguzi umeonesha kuwa vyanzo vilivyopelekea wateja waliokaguliwa kulalamika umeme kuisha kwa haraka ni uchakavu wa mtandao wa nyaya za umeme (wiring) ndani ya nyumba, hali iliyosababisha umeme kuvuja bila mtumiaji kugundua.

Aidha, matumizi holela ya umeme yameonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa changamoto hiyo.

Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Gowelle amesema“Baada ya kuona malalamiko yanaongezeka, tuliona ni muhimu kufika moja kwa moja kwa baadhi ya wateja waliolalamika. Tulifanya ukaguzi wa kitaalamu, tukazima vifaa vya umeme na kufuatilia usomaji wa mita, lakini bado uniti ziliendelea kupungua.

Hii ilithibitisha kuwepo kwa hitilafu katika mfumo wa wiring za ndani ya nyumba na sio mita.”Katika nyumba moja iliyopo Tabata, ukaguzi ulibaini kuwa uchakavu wa mtandao wa nyaya (wiring) ulisababisha upotevu wa takribani uniti mbili za umeme, hali iliyomfanya mteja kutumia zaidi ya shilingi 30,000 za ziada kwa mwezi kuliko matumizi yake halisi.

Kwa upande mwingine, katika nyumba ya mteja mmoja eneo la Kimara Suka, timu ya ukaguzi ilishuhudia matumizi yasiyo bora ya umeme, ikiwemo kuwasha taa wakati wa mchana, hali iliyotajwa kuweza kuchangia kuisha kwa umeme.

Wateja Waliokaguliwa

Miongoni mwa wateja waliokaguliwa ni Devotha Kihwelo, mwandishi wa Gazeti la Mwananchi na mkazi wa Tabata, ambaye taarifa yake iliifanya TANESCO kuwajibika kwa kuchukua hatua ya kufanya ukaguzi huo ambapo Baada ya uchunguzi, ilibainika kuwa nyumba aliyokuwa akiishi ilikuwa na hitilafu kwenye wiring ambayo ilikua ya muda mrefu hali iliyosababisha umeme kupotea.

Wateja wengine waliokaguliwa ni John Vincent wa Tabata Kimanga na Crispin Mizambwa wa Kimara Suka. Kwao, ukaguzi umebaini kuwa mita zao zilikuwa hazina changamoto yoyote, na matumizi yao ya wastani wa uniti 2–3 kwa siku yaliendana na vifaa walivyokuwa wakitumia.

Kutokana na matokeo hayo, TANESCO ilijiridhisha kuwa madai ya kuisha kwa umeme bila sababu ya msingi hayakusababishwa na ubovu wa mita na kwamba mita zilikua salama na sawa kiutendaji.*

Ushauri kwa Wateja

TANESCO imetoa elimu ya sababu zinazoweza kuchangia umeme kuisha haraka kuwa ni pamoja na ; • Uchakavu wa mtandao wa nyaya za ndani ya nyumba (wiring) • Matumizi holela ya umeme • Matumizi ya vifaa vya zamani ,vilivyokaa muda mrefu au visivyo na ufanisi wa matumizi ya umeme kidogo • Kutotumia vifaa vyenye teknolojia ya matumizi fanisi (energy efficiency).

Gowelle amewashauri wateja kufanya jaribio rahisi la kujitathmini kabla ya kulalamika “Wateja wazime vifaa vyote vya umeme, wasome kiwango cha uniti, wakae kwa muda usiopungua saa nne, kisha wasome tena. Endapo uniti zitakuwa zimepungua, wawasiliane na TANESCO kwa ukaguzi.

Ikiwa hazijapungua, basi changamoto sio mita bali ni matumizi ya vifaa vyao au mfumo wa wiring zao za ndani umechoka.

Wito kwa Umma

TANESCO imetoa wito kwa wateja wote wanaokumbana na changamoto za umeme kuisha haraka kuwasiliana na Shirika moja kwa moja kwa msaada badala ya kuamini au kusambaza taarifa zisizothibitishwa , ili kufanyiwa ukaguzi na kupata ufumbuzi wa kitaalamu unaolenga kupunguza gharama zisizo za lazima kwa wateja wake.

spot_img

Latest articles

Vijana Dar wakutana kusherehekea kumbukizi ya kuzaliwa Rais Samia, wasifu mchango wake kwa maendeleo ya vijana

Na Mwandishi Wetu VIJANA Jijini Dar es Salaam wameungana kusherehekea siku ya kumbukizi ya...

Twiga, Tanga Cement wapewa saa 48 kujisalimisha

Na Mwandishi Wetu SERIKALI kupitia Wizara ya Madini imezipa Kampuni za Twiga Cement na...

Watendaji wa Uchaguzi watakiwa kutekeleza majukumu kwa weledi

Na. Mwandishi Wetu, Iringa WATENDAJI wa uchaguzi wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi...

Kipa wa zamani Yanga afariki dunia

Na Winfrida Mtoi KIPA wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania, Peter...

More like this

Vijana Dar wakutana kusherehekea kumbukizi ya kuzaliwa Rais Samia, wasifu mchango wake kwa maendeleo ya vijana

Na Mwandishi Wetu VIJANA Jijini Dar es Salaam wameungana kusherehekea siku ya kumbukizi ya...

Twiga, Tanga Cement wapewa saa 48 kujisalimisha

Na Mwandishi Wetu SERIKALI kupitia Wizara ya Madini imezipa Kampuni za Twiga Cement na...

Watendaji wa Uchaguzi watakiwa kutekeleza majukumu kwa weledi

Na. Mwandishi Wetu, Iringa WATENDAJI wa uchaguzi wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi...