Na Mwandishi Wetu
SERIKALI kupitia Wizara ya Madini imezipa Kampuni za Twiga Cement na Tanga Cement saa 48 kufika mbele ya mamlaka husika na kujibu hoja zinazowakabili, ikiwemo madai ya kukiuka bei elekezi za madini zinazotolewa na Serikali na kukosa mikataba kwa wauzaji wa malighafi viwandani.
Akizungumza leo katika kikao cha wachimbaji wadogo wa madini ya Jasi (gypsum) kutoka Same mkoani Kilimanjaro kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Gold, Ofisi za Tume ya Madini jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amesema kampuni hizo zikikaidi wito huo, Serikali itachukua hatua kali ikiwemo kusimamisha shughuli zao.

“Kitendo cha kukaidi wito wa Serikali ni kuidharau mamlaka. Wasipofika ndani ya saa 48, tutamshauri Waziri kufuta leseni zao,” amesema Mhe. Dkt. Kiruswa.
Amesisitiza kuwa kampuni hizo zinapaswa kulipa wasambazaji wa madini ya jasi kwa kuzingatia bei elekezi iliyowekwa na Serikali, kutoa mikataba ya kazi kwa wauzaji wa bidhaa, na kuacha kununua kwa bei ya chini inayowaumiza wachimbaji wadogo.
Kauli hiyo imekuja kufuatia malalamiko ya wachimbaji wadogo wa madini ya jasi wa Wilaya ya Same, wakidai kuwa kampuni hizo zinakinyima kazi Chama cha Ushirika cha Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Jasi (Kilimanjaro Gypsum Cooperative Society Ltd), na badala yake kushirikiana na watu binafsi wachache wanaolipwa chini ya bei elekezi na bila mikataba.

“Mnaokubali kuuza madini yenu kwa bei ya chini mnajipiga misumari wenyewe. Bei elekezi iheshimiwe,” amesisitiza Dkt. Kiruswa, huku akiwataka wachimbaji kutulia wakati Serikali ikishughulikia changamoto hiyo.
Aidha, Naibu Waziri amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, kuipeleka TAKUKURU kuchunguza madai ya rushwa yanayodaiwa kujitokeza katika viwanda hivyo.
Awali, Kamishna wa Tume ya Madini, Dkt. Theresia Numbi, amesema utoaji wa mikataba ni takwa la kisheria, si hiari.

“Ni lazima Chama cha Ushirika kishirikishwe. Toeni asilimia kwa Chama, na nyingine muwape wale mnaowataka kufanya nao kazi,” amesema.
Kwa upande wake, Meneja Uwezeshaji Uchimbaji Mdogo, Nchagwa Marwa, kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) amesema uchimbaji ni sekta jumuishi, akiongeza kuwa kuwa kumpendelea mtu mmoja na kukiacha Chama si mwelekeo sahihi.
“Msimamo wa Serikali ni kila Mtanzania anufaike na rasilimali madini. Ndiyo maana kauli mbiu ni Madini ni Maisha na Utajiri. Bei elekezi iheshimiwe,” amesema.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, amezitaka kampuni kufuata taratibu za utoaji wa oda akisisitiza kuwa Serikali inatoa upendeleo kwa wazawa na matarajio ni wawekezaji kuwalinda wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, amelaani vikali hatua ya kampuni hizo kudharau wito wa Serikali, akidai hali ya usalama katika maeneo ya Makanya na Ruvu Kajiungeni imeathirika kutokana na mgawanyiko miongoni mwa wachimbaji.

“Viongozi wote tumekuja, Madiwani, Mkurugenzi, Katibu Tawala wa Wilaya kwa lengo la kumaliza mgogoro na kurejesha amani. Kudharau huku ni kudharau Serikali na hata dhamana ya Mheshimiwa Rais. Wizara ichukue hatua stahiki, hata ikibidi kuzisimamisha shughuli za viwanda hadi suluhu ipatikane,” amesema.
Serikali imesisitiza itaendelea kulinda maslahi ya wachimbaji wadogo, kusimamia bei elekezi, na kuhakikisha sekta ya madini inakuwa jumuishi kwa manufaa ya Watanzania wote.


