Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba amesema Serikali inataka kazi zote zifanyike makao makuu ya nchi Dodoma ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
Ameyasema hayo leo Januari 22, 2026, alipotembelea ofisi za Wizara ya Maji na Wizara ya Madini zilizopo mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma.
“Ninawapongeza sana mmehamia Makao Makuu. Taasisi zote za Serikali zinapaswa kutambua kwamba makao makuu ya nchi ni Dodoma, na huduma zote zinapaswa kutolewa hapa. Hii sio kambi na wala hatutakuwa na makao makuu mbili zilizo sambamba,” amesema Waziri Mkuu.

Pia, ameziagiza taasisi zote ambazo zimeshakamilisha ujenzi wa majengo katika makao makuu kuyatoa majengo hayo kwa taasisi ambazo haziwajibiki kuhamia Dodoma lakini bado zimepanga.
“Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, mwelekeze Katibu Mkuu atengeneze timu ifanye tathmini ya majengo yote ya Serikali yaliyoko Dar es Salaam ambayo hayana matumizi ili tuyagawe kwa taasisi nyingine ambazo zimepanga. Angalia Serikali ina majengo yasiyotumika,” ameagiza Dk. Mwigulu.
Akizungumza na watumishi wa Wizara ya Maji, Waziri Mkuu amewataka kuchukua hatua za kukomesha upotevu wa maji.


