Na Mwandishi Wetu
MWASISI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mzee Edwin Mtei anatarajiwa kuzikwa Jumamosi ya Januari 24, 2026 nyumbani kwake Tengeru nje kidogo ya Jiji la Arusha.
Mzee Mtei ambaye pia alikuwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), alifariki dunia usiku wa Jumatatu, Januari 19, 2026 jijini Arusha, akiwa na umri wa miaka 94.
Aidha viongozi mbalimbali wamefika nyumbani kwa marehemu akiwemo Mwenyekiti mstaafu wa Chadema Freeman Mbowe ambaye ni msemaji wa familia kwa sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ratiba ya mazishi, Mbowe amesema msiba wa Mzee Mtei ni wa kijamii na unawahusu watu wa makundi mbalimbali ndani na nje ya siasa, kutokana na mchango wake mkubwa katika historia ya Tanzania, hivyo waombolezaji kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kushiriki mazishi hayo.
“Huu ni msiba shirikishi. Kwanza huyu ni senior citizen aliyelitumikia taifa tangu kipindi cha uhuru na hata kabla ya uhuru. Huu si msiba wa mtu mmoja, ni msiba jumuishi unaowahusu wanasiasa na wasio wanasiasa,” amesema Mbowe.


