📍 Kamati yaipongeza TAWA kwa ubunifu uliopelekea ongezeko la watalii, mapato
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Timotheo Mzanva (Mb) imeipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa ubunifu wake katika sekta ya uhifadhi na utalii, ubunifu uliosababisha ongezeko kubwa la watalii na mapato ya Serikali.
Pongezi hizo zimetolewa baada ya Kamati kupokea wasilisho la utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo.Taarifa ya TAWA iliwasilishwa leo Januari 21, 2026 jijini Dodoma na Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mlage Yussuf Kabange kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), katika mwendelezo wa Wizara hiyo kuwasilisha taarifa za taasisi zake kwa Kamati ya Bunge.

Katika wasilisho hilo, Kamishna Kabange aliieleza Kamati kuwa TAWA inasimamia eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 133,286.36, linalojumuisha Mapori ya Akiba 28, Mapori Tengefu 23, Maeneo ya Malikale 2, Bustani za ufugaji wa wanyamapori za Serikali 5, Hifadhi ya Makuyuni Wildlife Park na Kisiwa cha Lundo, ambapo juhudi za kuimarisha ulinzi na kudhibiti ujangili zimechangia kuongezeka kwa idadi ya wanyamapori katika maeneo hayo.
Aidha, Kabange alibainisha juhudi zinazochukuliwa na taasisi hiyo kutatua migogoro ya mipaka kati ya hifadhi na makazi ya wananchi, akisema TAWA kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, TAMISEMI pamoja na mamlaka za mikoa na wilaya imefanikiwa kuweka alama za mipaka 3,192 na kulipa fidia kwa wananchi waliopisha maeneo ya hifadhi, hususan katika Pori la Akiba la Kilombero.

Katika hatua ya kuongeza mapato na kuboresha uhifadhi, Kamati ilielezwa kuhusu kuanzishwa kwa Makuyuni Wildlife Park, hatua iliyosaidia kuimarisha ulinzi, kuboresha miundombinu na kuvutia wawekezaji wa utalii, huku hifadhi hiyo ikichangia mapato ya zaidi ya shilingi milioni 315 katika mwaka wa fedha 2024/25.
Sambamba na hilo, Kabange aliieleza Kamati kuwa hadi sasa TAWA imesaini mikataba 13 ya uwekezaji mahiri na mikataba mitatu ya uwekezaji wa huduma za malazi, ambayo inatarajiwa kuiingizia Serikali mapato ya wastani wa dola za Marekani 27,111,329 kwa mwaka, huku shilingi bilioni 12.2 zikikusanywa katika mwaka wa fedha 2024/25 kutokana na mikataba hiyo.

Kwa upande wa ushirikishwaji wa jamii, TAWA imeendelea kuwahusisha wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi katika shughuli za uhifadhi ikiwemo ufugaji nyuki na uvuvi, ambapo gawio na stahiki zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 22.63 zimetolewa kwa wanufaika wa shughuli za utalii.
Kaimu Kamishna huyo pia aliieleza Kamati kuwa utalii wa uwindaji umeimarika kutokana na maboresho ya sera yaliyowezesha uwindaji kufanyika kwa mwaka mzima na kuongeza muda wa umiliki wa vitalu, huku utalii wa picha ukishuhudia ongezeko la watalii kutoka 37,684 mwaka 2020/21 hadi kufikia 240,967 mwaka 2024/25.

Akihitimisha kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mzanva (Mb), aliipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na taasisi zake, akisema mafanikio ya TAWA yanaonesha umuhimu wa uwekezaji na ubunifu katika kulinda rasilimali za Taifa na kuongeza mapato kupitia sekta ya utalii.
Aidha, kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hassan Chande (Mb), Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Hassan Abbasi, Naibu Katibu Mkuu, Bw. Nkoba Mabula, pamoja na viongozi wa menejimenti ya Wizara na wakuu wa taasisi na vyuo vilivyo chini ya Wizara hiyo.


