Na Mwandishi Wetu
FAMILIA ya aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, leo Jumanne, Januari 6, 2026, imefika katika nyumba aliyokuwa akiishi eneo la Ununio jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukusanya mali zake, pamoja na kufanya maombi kwenye nyumba aliyokuwa akiishi.
Ndugu hao wakiongozwa na mama mzazi wa Humphrey Polepole, Mama Anna Marry Polepole na mdogo wake Godfrey Polepole, wamesema wataendelea kumuombea ndugu yao na kuisihi jamii kuendelea kushirikiana na vyombo husika pale taarifa zozote zitakapopatikana
Akizungumza na waandishi wa habari, Mama wa Polepole ameeleza kuwa wamekwenda kutoa vitu katika nyumba hiyo aliyokuwa amepanda mwanaye kwa sababu hakuna anayeweza kulipa kodi.
Amesisitiza kuwa anaomba waliomchukua mtoto wake wamrudishe akiwa mzima na ikiwa ana makosa aliyofanya ashtakiwe kama wengine.
Polepole, ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini alidaiwa kutekwa na watu wasiojulikana miezi mitatu iliyopita na hadi sasa hatima yake ikiwa bado haijulikani rasmi.


