Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itayaendeleza mambo yote mema yaliyofanywa na aliyekuwa mbunge wa Peramiho mkoani Ruvuma, marehemu Jenista Mhagama ikiwemo kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za kidini.
Ameitoa kauli hiyo leo Jumatatu, Desemba 15, 2025, wakati akiwasilisha salamu za Serikali aliposhiriki Ibada ya kuaga mwili wa Marehemu Jenista iliyofanyika katika kanisa Katoliki la Abasia ya Mtakatifu Benedicto, Peramiho.
Dk. Mwigulu amesema marehemu Jenista alikuwa mpatanishi akiunganisha makundi mbalimbali yakiwemo ya wafanyakazi na Serikali ambapo hadi leo wanaushirikiano mkubwa, pia aliimarisha umoja na mshikamano kati ya Serikali na sekta binafsi na alifanya kazi hiyo kwa uadilifu mkubwa.

“Marehemu Jenista amekuwa anaamini katika mafanikio na hiyo ndio iliyompa jina la kiraka kwa kuwa kila nafasi aliyopewa aliimudu kwa ukamilifu. Jenista amegusa maisha ya wengi, mimi nilikuwa nashirikiana naye katika masuala ya uongozi na alikuwa mmoja wa marafiki wa familia,”
Katika salamu hizo, Waziri Mkuu amesema kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amemuagiza awahakikishie Watanzania wakiwemo Wanaruvuma kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao kama ilivyokuwa inafanya wakati wa uhai wa Jenista.

“Mheshimiwa Jenista alikuwa kiungo kati ya Wana-Ruvuma na Wana-Peramiho na alikuwa kiungo kati ya Kanisa na Serikali, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amenituma niwahakikishie wote kwamba Serikali itaendelea kuyaenzi mema yote aliyoyafanya enzi za uhai wake,” amesema.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahakikisha watoto wa marehemu kwamba hawatakuwa peke yao, wataendelea kushirikiana nao, ambapo amewasisitiza watoto hao waendelee kumtanguliza Mwenyezi Mungu mbele huku wakishikamana na kupendana somo ambalo marehemu amewaachia.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Mussa Zungu amewashukuru viongozi wa Serikali na viongozi wa dini kwa kazi kubwa waliyoifanya tangu kutokea kwa msiba.
Awali Victor Mhagama ambaye ni mtoto wa marehemu ameishukuru Serikali kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa familia tangu kutokea kwa msiba huo huku akiiomba Serikali na wananchi kwa ujumla waendelee kuwa pamoja nao.


