Mwanadiplomasia nguli wa Tanzania, aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Nigeria na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Eswatini na Namibia, Timothy Bandora (72), anatarajia kuzikwa kesho Desemba 16, 2025, katika Makaburi ya Kinondoni.
Balozi Bandora alifariki dunia wiki iliyopita akiwa jijini Nairobi, nchini Kenya, ambako alikuwa akipatiwa matibabu.
Aliitumikia Serikali kuanzia awamu ya kwanza hadi ya tatu, alitekeleza majukumu mbalimbali ya kitaifa na kimataifa katika utumishi wa umma pamoja na ndani ya Umoja wa Mataifa (UN), akihudumu katika nyadhifa tofauti kwa uadilifu na weledi mkubwa.
Kwa mujibu wa ratiba ya msiba iliyotolewa na familia, ibada ya mazishi itafanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Msasani, jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa majukumu aliyofanya wakati wa uhai wake ni kuongoza kurugenzi ya ushirikiano wa kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi wa Tanzania nchini Nigeria ofisi ya Lagos, ambayo pia inahudumia nchi za Benin, Togo, Cote d’Ivoire, Ghana, Guinea, Senegal, Burkina Faso, Mali, Sierra Leone, Liberia, Guinea-Bissau na Mauritania.


