Prof. Mkenda: Serikali imeendelea kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya Elimu

Na Tatu Mohamed

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Serikali imeendelea kufanya mageuzi katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuimarisha mpango wa kurasimisha ujuzi wa vijana waliopata stadi mbalimbali nje ya mfumo rasmi wa elimu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Disemba 10, 2025 jijini Dar es Salaam, Prof. Mkenda amesema mpango huo unalenga kufungua fursa zaidi za ajira kwa vijana kupitia tathmini ya kazi wanazozifanya na kuwapatia vyeti baada ya wataalamu wa Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA) kupima kiwango cha ujuzi wao.

“Kuna utaratibu tumekuwa tukiufanya na sasa tunaendelea kuuimarisha. Ukifika VETA, wataalamu watakupima ujuzi na baada ya hapo utapata cheti kitakachokuwezesha kupata kazi,” amesema.

Waziri Mkenda amesema juhudi hizo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kujenga nguvu kazi yenye ujuzi wa vitendo, hususan kwenye maeneo ya sayansi, teknolojia na viwanda.

Ameongeza kuwa Serikali imeweka msisitizo mkubwa kwenye masomo ya sayansi, teknolojia na ubunifu ili nchi iweze kusonga mbele kiuchumi.

“Chini ya maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kila mkoa umejengewa Sekondari ya Wasichana ya Sayansi. Lengo ni kuhakikisha vijana wenye uwezo hawakatishwi tamaa kwa changamoto za kifedha,” ameeleza.

Amesema Serikali inaendelea kusomesha bure vijana wote wenye uwezo wa kusoma masomo ya sayansi, na mpango wa kujenga shule maalum za wavulana za sayansi unaendelea.

Akizungumzia miradi ya maendeleo kwa mwaka 2025/2026, Prof. Mkenda amesema sekta ya elimu imepata mageuzi makubwa kufuatia kuongezeka kwa bajeti ya elimu kwa asilimia 40, kutoka trilioni 5.3 hadi trilioni 7.4.

Amesema ongezeko hilo limewezesha maandalizi ya wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira ndani na nje ya nchi, sambamba na kupanua miundombinu na kuboresha mazingira ya kujifunzia.

“Nchi haiwezi kusonga mbele bila uwekezaji mkubwa katika sayansi, teknolojia na ubunifu. Ndiyo maana Serikali inaongeza nguvu katika maeneo haya,” ameongeza.

Katika kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia duniani, Prof. Mkenda amesema Serikali imeanza kuwekeza katika mafunzo ya Artificial Intelligence (AI) na Data Science kwa vijana.

Amesema hadi sasa vijana 50 tayari wamechukuliwa kwenye kambi maalumu ya maandalizi, ambapo kundi la kwanza litaondoka Januari kwenda Afrika Kusini, na kundi la pili kwenda Ireland mwezi Septemba kwa ufadhili wa Serikali.

Waziri Mkenda pia amegusia changamoto ya wanafunzi kuacha shule, akisema utafiti wa Wizara umebaini kuwa Mkoa wa Geita unaongoza kwa idadi kubwa ya wanaoacha shule kutokana na shughuli za madini na changamoto za kifamilia.

Kutokana na hilo, Wizara imeanzisha mfumo unganishi utakaofuatilia kila mwanafunzi tangu anapoanza elimu hadi anapomaliza.

“Mfumo huu utamfuatilia mwanafunzi popote alipo. Hata akiacha shule, tutajua sababu na kuchukua hatua,” amesema.

Katika hatua nyingine, amesema Serikali inatekeleza ahadi ya Rais Samia ya kutoa ajira mpya za walimu, ambapo jumla ya walimu 7,000 wanatarajiwa kuajiriwa ndani ya siku 100 zijazo.

“Ajira zimeshatangazwa, na walimu watakaopatikana watapelekwa mara moja kwenye vituo vya kazi,” amesema.

spot_img

Latest articles

Tumeepuka balaa jingine, uadilifu uongoze tiba machungu ya MO29

JUMANNE wiki hii Watanzania walisherehekea siku ya uhuru wa Tanganyika wengi wakiwa majumbani kwao....

Aweso aridhishwa na wingi wa maji Ruvu Juu, aipa Dawasa jukumu

Na Mwandishi Wetu WAZIRI wa maji, Jumaa Aweso amekagua na kujiridhisha na wingi wa...

Jeshi la Polisi latoa onyo wanaondelea kuhamasisha maandamano

Na Mwandishi Wetu JESHI la Polisi nchini limesema  kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi...

Watanzania waaswa kudumisha amani, Umoja na mshikamano

Na Mwandishi Wetu KATIKA kuadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Tanganyika, Watanzania wametakiwa kukumbuka...

More like this

Tumeepuka balaa jingine, uadilifu uongoze tiba machungu ya MO29

JUMANNE wiki hii Watanzania walisherehekea siku ya uhuru wa Tanganyika wengi wakiwa majumbani kwao....

Aweso aridhishwa na wingi wa maji Ruvu Juu, aipa Dawasa jukumu

Na Mwandishi Wetu WAZIRI wa maji, Jumaa Aweso amekagua na kujiridhisha na wingi wa...

Jeshi la Polisi latoa onyo wanaondelea kuhamasisha maandamano

Na Mwandishi Wetu JESHI la Polisi nchini limesema  kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi...