Na Mwandishi Wetu
JESHI la Polisi nchini limesema kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama litaendelea kuimarisha hali ya usalama nchini na kulinda maisha ya wananchi na mali zao, huku likionya wale wanaondelea kuhamassha maandamano.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime leo Disemba 10, 2025, limeonya wale wanaopanga kujitokeza leo kwenye mitaa mbalimbali ili kufanya kile kinachoitwa maandamano ya amani kutokana na kushindwa kuyafanya jana Desemba 9, 2025.
“Jeshi la Polisi linaendelea kuwakumbusha, kuwasisitiza na kuwaonya wasifanye hivyo kwani wanachokiita maandamano ya amani yasiyo na kikomo yalipigwa marufuku kutokana na kukosa sifa kulingana na matakwa ya Katiba na sheria ya Polisi na Polisi wasaidizi sura 322,” amesema Misime.
Amesema kuwa kwa atakayekaidi kutii sheria za nchi kwa lengo la kuhatarisha usalama wa nchi ili kusimamisha shughuli za kiuchumi na kijamii zisiendelee, watadhibitiwa ili nchi ibaki salama na watanzania wema na wapenda amani wabaki salama.
Aidha taarifa hiyo imetoa wito kwa wananchi kuendelea kufanya shughuli zao na kufuata maelekezo watakayokuwa wanapewa na vyombo vya ulinzi na usalama katika maeneo yote nchini sambamba na kutii sheria za nchi.


