RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa vurugu zilizotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 zilikuwa na viashiria vya kupindua dola, hivyo akatetea hatua zilizochukuliwa na vyombo vya dola kukabiliana na maandamano na vurugu, matukio ambayo yaliripotiwa kusababisha vifo na majeruhi.
“Serikali ililazimika kuchukua hatua za haraka kulinda usalama wa raia na nchi, kwa mujibu wa kiapo changu cha kuilinda Jamhuri,” amesema Rais Samia alipokuwa akilihutubia Taifa kupitia mkutano wa Wazee wa mkoa wa Dar es Salaam na kuongeza:
“Nguvu iliyotumika inaendana na tukio lililopo, tunapoambiwa kwamba tumetumia nguvu kubwa sana kwenye tukio lile, nguvu ndogo ilikuwa ipi?” ilikuwa tuwaangalie waandamanaji waliojiandaa kufanya mapinduzi mpaka wafanikiwe, hapo patakuwa na dola kweli? dola haiko hivyo”
Rais Samia amesema vurugu hizo zilihusisha vijana wengi waliokuwa wanafuata mkumbo bila kuelewa madhara yake, lakini nyuma yake kulikuwa na nia ovu ya kuvuruga amani ya nchi, ambayo ilichochewa na mataifa ya nje ambayo alisema yanaionea wivu Tanzania kutokana na uzuri wake.
“Wanaporudi kutulaumu kwamba tumetumia nguvu kubwa, wao walitaka nini, tujiulize Je hao ndiyo wafadhili wa kile kilichofanyika, walitaka tuangalie ile mob (kundi) mpaka lifanikiwe walichowapa fedha, walichowatuma, hapana!,” alisema Rais Samia.
Amesema mataifa hayo (ambayo hakuyataja) yamekuwa yakihoji kile kilichotokea Tanzania kana kwamba katika nchi hizo huwa hazina matukio ya aina hiyo. “…kwao hayatokei, wanadhania wao ni wakoloni kwetu, ni kitu gani? ni fedha chache wanayotugaia?,”alihoji Rais Samia.
Kuhusu maandamano mengine yanayotajwa kupangwa kufanyika Desemba 9, 2025, Rais amesema Serikali imejipanga. “likija wakati wowote tumejipanga….tutasimama na kuilinda nchi hii kwa nguvu zote,” amesema.
Maridhiano
Rais Samia aliwahakikishia wazee hao kwamba Serikali itaendelea kufungua milango ya mazungumzo, lakini kwa misingi ya utulivu, kuheshimiana na kutambua mamlaka ya kikatiba ya pande zote.
Hata hivyo amesema Serikali yake haitakubali kuamrishwa, kuwekewa masharti, au kuongozwa namna ya kuendesha majadiliano na wadau wa siasa, akisisitiza kuwa Tanzania ni taifa huru linalofanya maamuzi kwa mujibu wa mamlaka yake kamili.
Katika mkutano huo uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Rais Samia amesema kumekuwepo watu wanaotoa masharti kabla ya kukubali kushiriki mazungumzo ya maridhiano.
“Serikali hii si ya kuamrishwa wala kupewa maelekezo. Mazungumzo tunayoyataka ni ya kuheshimiana na kutambua nafasi ya kila upande, si ya kutuambia ‘mfanye hili’ au ‘mwachieni huyu’ kabla ya kukaa mezani.
“Wanadamu hukosana na wakaelewana…inawezekana kabisa kuna mapungufu na hakuna serikali yoyote duniani isiyo na mapungufu lakini wanakaa, wanazungumza na kuondoa mapungufu yaliyopo,” amesema.
Viongozi wa dini
Kadhalika Rais Samia amegusia nafasi ya viongozi wa dini katika masuala ya kitaifa, akionya dhidi ya kuingilia mipaka ya majukumu ya kikatiba.
Amesema ingawa Watanzania wanafuata dini mbalimbali, Katiba haiipi dini au dhehebu lolote mamlaka ya kutawala au kuathiri uendeshaji wa nchi.
“Viongozi wa dini msijivishe majoho ya kwamba nyinyi ndiyo mnaweza ‘kuover run’ nchi hii—hakuna. Tutafuata Katiba na Sheria. Hakuna dini itakayotoa tamko na likaigeuza Tanzania,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa baadhi ya taasisi za dini zimekuwa zikitoa matamko yanayotofautiana kwa ndani, hivyo si sahihi kuyatumia kama msingi wa kuiongoza nchi, huku akilitaja moja kwa moja Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
“Mimi toka nimekaa, matamko 8 yametolewa na TEC lakini ukienda chini wenyewe wanapingana,” amesema.
Rais ameitaja taassi hiyo ikiwa ni siku moja tangu Katibu Mtendaji wa chombo hicho kikuu cha Kanisa Katoliki nchini, Padre Dkt. Charles Kitima aliposema Serikali inapaswa kukiri kwamba katika matukio ya Oktoba 29 kulikuwa na vifo vilivyosababishwa na risasi.
“Tukiri kwamba watu wameuawa kwa kupigwa risasi za moto. Hatujaongelea watu waliokatwa mapanga sijui kama wapo hatujui, polisi watatuambia au labda hiyo Tume itasema. Kwa hiyo hakuna suala kwamba labda tusubiri Tume. Tukiri ukweli,”alisema Katibu huyo wa TEC na kuongeza:
“Kwanza kuunda Tume ni ishara kwamba ukweli fulani unafahamika, ila hutaki kutajwa, na Watanzania hawa milioni 70 wanataka kusikia neno, watu wameuawa, tunakiri kutokea mauaji ya kutumia silaha za moto kwa kutumia risasi. Sasa ni nani, ndiyo hiyo Tume ije ituambie, sababu huenda kuna watu walivaa yale mavazi huenda hawakuwa polisi sijui nani, sasa hiyo sisi tusiingilie sana.”
Kadhalika Padre Kitima alizungumzia majeruhi waliofikishwa katika hospitali zinazoendeshwa na Kanisa Katoliki akisema: “Sisi tunamiliki hospitali, hapa Ukonga hapa Kardinali Rugambwa, askari anaenda pale anamwambia Sister, ‘usiwatibu hawa tunataka tuwaone kwenye mochwari, usiwatibu hawa walikuwa wanaleta vurugu’.
“Mtu ameenda ameumia amepigwa risasi, lazima tumtibu halafu baadaye sheria zinaruhusu hata kama hana PF3 tunaruhusiwa kumtibu halafu baadaye tutahakikisha tunatoa taarifa polisi kwamba mtu huyu hapa alikuja amepigwa risasi, hatujui nani amempiga lakini tumeona tuokoe maisha yake kwasababu cha kwanza lazima tuokoe maisha.”


