Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema kuwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme kwa ufanisi mkubwa, hatua inayoliwezesha taifa kusonga mbele katika kujenga mfumo madhubuti wa upatikanaji wa nishati ya umeme.
Mhe. Ndejembi amesema hayo Novemba 27, 2025, wakati wa ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma, ambapo ametaka kuona kazi inakamilika kwa wakati na viwango vinavyotakiwa.

Mhe. Ndejembi amebainisha kuwa mradi huo mkubwa unatekelezwa kwa fedha za ndani, na hadi kukamilika kwake utagharimu takribani shilingi bilioni 556.
“Niwaagize TANESCO kuendelea kumsimamia Mkandarasi kuhakikisha kazi inakamilika kulingana na ratiba. Hatutaki kufika mwisho wa utekelezaji na kukuta mradi umekabidhiwa bila kukamilika,” amesisitiza Waziri Ndejembi.
Ameongeza kuwa TANESCO imeelekezwa kukutana na Mkandarasi ili kuandaa mpango kazi mpya utakaoonesha mikakati ya ufuatiliaji wa hatua kwa hatua katika ukamilishaji wa mradi huo muhimu kwa taifa.

Aidha, Waziri Ndejembi amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatoa msukumo mkubwa kuhakikisha umeme unawafikia wananchi kote nchini kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amesema Tanzania ina umeme wa kutosha kutoka kwenye vyanzo vyake vya uzalishaji, na kazi kubwa inayoendelea sasa ni kuutoa umeme huo katika maeneo ya uzalishaji na kuufikisha kwa wananchi na wawekezaji.

Bw. Twange ameeleza kuwa Serikali imekamilisha ujenzi wa vituo vikubwa vya kupokea na kupoza umeme katika Dodoma na Chalinze, ambavyo vitakuwa kitovu cha kusafirisha umeme kutoka Mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) na vyanzo vingine kwenda maeneo mbalimbali ya nchi.
“Kituo cha kupokea umeme cha Dodoma ni njia panda muhimu inayopokea umeme kutoka maeneo mbalimbali, na pia ndicho kinachotuunganisha na wenzetu nchini Kenya,” amesema BW. Twange
Ameongeza kuwa hatua hizi zote ni muhimu katika kulifanya taifa kuwa na mfumo imara wa umeme unaokidhi mahitaji ya sasa na ya vizazi vijavyo.


