Na Mwandishi Wetu
Watuhumiwa 20 kati ya 22 waliokuwa wanashtakiwa kwa makosa ya uhaini wameachiwa huru, huku mfanyabiashara wa vipodozi Jenifer Jovin (26) maarufu Niffer na Mika Lucas Chavala kurudishwa rumande.
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) amewafutia kesi hiyo ya uchunguzi namba 26388/ 2025 chini ya kifungu namba 92(1) cha Sheria ya Makosa ya Jinai, Sura ya 20 ilivyofanya marejeo mwaka 2023.
Uamuzi wa kuwafutia kesi hiyo kwa washtakiwa 20, umetolewa leo Jumanne, Novemba 25, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Aaron Lyamuya, baada ya Wakili wa Ssrikali, Titus Aron kuieleza Mahakaka hiyo kuwa DPP hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa 20 kati ya washtakiwa 22 wanakabiliwa na kesi hiyo.
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Novemba 7, 2025. Kuachiwa huru kwa baadhi ya watuhumiwa kumekuja kutokana na kauli ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwamba wale waliofuata mkumbo wakati wa vuguvugu za siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025 iangaliwe namna ya kuachiwa.


