Na Mwandishi Wetu
Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba ameagiza kufunguliwa kwa Kanisa la Ufufuo na Uzima, huku akielekeza lipewe miezi sita ya uangalizi katika kuzingatia miiko, masharti na sheria za uendeshwaji wake.
Waziri Dk. Mwigulu amesema hayo wakati akizungumza na wakazi wa Kimara na Mbezi Luis Jijini Dar es Salaam leo November 24, 2025 akiwa katika ziara ya kukagua uharibifu uliotokea katika kipindi cha maandamano na vurugu zilioanza Oktoba 29, 2025 siku ya uchaguzi mkuu.
Ameelekeza kurekebishwa kwa sharti linalotaka kufungiwa kwa nyumba ya ibada iwapo atakosea kiongozi, akisisitiza anayekosea ndiye aadhibiwe bila kuathiri waumini kufanya ibada.
“Natambua ilikuwepo hii moja ya Ufufuo na Uzima kaifungulie, ifungulie wape masharti ya uangalizi ndani ya miezi sita. Ziandikie taasisi zote za kidini kuzikumbusha miiko na mipaka ya ufanyaji kazi, sawa sawa na sheria na Katiba ya nchi yetu.
“Rais Samia ametoa msamaha kwenye Taasisi za kidini ambazo zilikuwa na msukosuko wa hapa na pale, Mh. Waziri wa Mambo ya ndani upo hapa, baada ya hapa fuatilia utaratibu mzuri ziandikie upya Tasisi za kidini, miiko yao, masharti yao ya uandikishwaji yanafikia wapi na zile ambazo zilikuwa na shida shida wape uangalizi wa miesi sita,” ameagiza Dk. Mwigulu.
Kanisa hilo lilikuwa chini ya Josephap Gwajima, lilifutiwa usajili, Juni 2, 2025 kutoka na kukiuka masharti ya uendeshaji wake, kwa kuhusisha siasa ndani yake.


