Na Tatu Mohamed
JUMLA ya watahiniwa 595,816 wamesajiliwa kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne 2025 unaotarajiwa kuanza kesho Oktoba 17, 2025 ambapo kati yao 569,914 ni watahiniwa wa shule na 25,902 ni watahiniwa wa kujitegemea.
Kati ya Watahiniwa wa Shule 569,914 waliosajiliwa mwaka 2025, wavulana ni 266,028 sawa na asilimia 46.68 na wasichana ni 303,886 sawa na asilimia 53.32.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 16, 2025, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania, Prof. Said Mohamed amesema wapo watahiniwa wa shule 1,128 wenye mahitaji maalum ambapo kati yao wenye uofu hafifu 860, wasioona ni 70, uziwi 58, wenye ulemavu wa akili ni 05 na wenye ulemavu wa viungo ni 135.

“Kati ya Watahiniwa wa kujitegemea 25,902 waliosajiliwa, wavulana ni 10,862 sawa na asilimia 41.93 na wasichana ni 15,040 sawa na asilimia 58.07. Aidha wapo watahiniwa wa Kujitegemea wenye mahitaji maalum 56, kati yao wenye uoni hafifu ni 49 na wasioona ni 7,” amesema.
Amefafanua kuwa maandalizi yote kwaajili ya kuendesha Mtihani huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa mitihani, vijitabu vya kujibia na nyaraka zote muhimu zinazohusu Mtihani katika Halmashauri/ Manispaa zote Tanzania Bara na Zanzibar.
Hata hivyo, ametoa wito kwa Kamati za Mitihani za Mikoa na Halmashauri zihakikishe kuwa usalama wa vituo vya Mitihani unaimarishwa na kwamba vituo hivyo vinatumika kwa kuzingatia mwongozo uliotolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania.

“Baraza linatoa wito kwa wasimamizi wote walioteuliwa kusimamia Mtihani huo kufanya kazi yao ya Usimamizi kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu. Wahakikishe wanafanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia kanuni za Mitihani na miongozo waliyopewa ili kila mtahiniwa apate haki yake,” amesema.
Aidha Baraza limewataka wamiliki wa Shule kutambua kuwa shule zao ni vituo Maalum vya Mitihani na hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote kuingilia majukumu ya wasimamizi wa Mtihani katika kipindi chote cha ufanyikaji wa Mtihani huo.
“Baraza la Mitihani Tanzania linawaomba wadau wote wa elimu na wananchi wote kutoa ushirikiano wakati wa uendeshaji wa Mtihani ili watahiniwa wote wafanye Mtihani katika hali ya utulivu. Aidha, wadau na wananchi wote watoe ushirikiano katika kudhibiti vitendo vyovyote vya udanganyifu katika Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2025,” amesisitiza.


