Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametangaza kuundwa kwa Tume Maalumu ya Kuchunguza vurugu na ghasia zilizotokea Oktoba 29, 2025 wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Akitangaza uamuzi huo wakati wa hotuba ya ufunguzi wa Bunge la 13 leo Novemba 14, 2025 jijini Dodoma, Rais Samia amesema Tume hiyo inalenga kubaini chanzo cha tukio hilo na kuishauri Serikali katika hatua za kurejesha amani na maridhiano.
“Serikali imechukua hatua ya kuunda Tume ya kuchunguza yaliyotokea ili tujue kiini cha tatizo. Taarifa hiyo itatuongoza kujielekeza kwenye mazungumzo ya kuleta maelewano na amani,” amesema.
Kabla ya kuendelea na hotuba yake, Rais Samia aliwaongoza Wabunge na wageni waalikwa kusimama kwa dakika moja kuwaombea wananchi waliopoteza maisha katika ghasia hizo na kutoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao pamoja na kuwaombea majeruhi kupona haraka.
Aidha Rais Samia amevielekeza vyombo vya dola kuwasamehe wale wote walioshiriki katika vurugu za Oktoba 29 kwa kufuata mkumbo.
“Kuna wakati vijana hufuata mkumbo wa uhalifu kwa ushabiki. Natambua vijana wengi waliokamatwa hawakujua wanachofanya. Ninaviagiza vyombo vya sheria, hasa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, kuwatizama vijana waliofuata mkumbo na hawakudhamiria waweze kuwaachia,” amesema Rais Samia.
Mwisho


