Na Mwandishi Wetu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amezindua rasmi Baraza la 11 la Wawakilishi Zanzibar, huku akitoa mwelekeo wa Serikali katika kipindi cha pili cha utawala wake, akisisitiza dhamira ya kuendeleza maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa msingi wa amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.
Akizungumza leo Novemba 10, 2025, katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani, Unguja, Rais Mwinyi amesema Serikali itaendelea kutekeleza Ilani ya CCM 2025–2030, pamoja na ahadi za kampeni na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha kwanza cha Awamu ya Nane.
Amesema Serikali itaendeleza mageuzi ya kiuchumi kwa kuimarisha sekta za uzalishaji, uwekezaji, sekta binafsi, na matumizi ya teknolojia za kisasa, ikiwa na lengo la kuongeza ukuaji wa uchumi kutoka asilimia 7 hadi 10 kwa mwaka.
Pia kudhibiti mfumko wa bei chini ya asilimia 5, kuzalisha ajira mpya 350,000, na kuongeza kipato cha mwananchi hadi Dola 1,880 kufikia mwaka 2030.
Aidha, itatekeleza ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani, bandari za abiria Mpigaduri, Kizimkazi, Shumba na Wete, pamoja na boti mbili za kisasa za mwendo kasi zitakazohudumia safari kati ya Unguja, Pemba, Tanga na Dar es Salaam.
Katika sekta ya afya, Serikali itajenga hospitali nne za mikoa, kuendeleza ujenzi wa Hospitali ya Saratani Binguni, na kuboresha Hospitali ya Mnazi Mmoja, itajenga madarasa mapya 2,000, shule tatu za sekondari za wasichana kwa kila mkoa, chuo cha kisasa cha ualimu, na kuajiri walimu 7,691.
Baraza la Wawakilishi Zanzibar linatarajiwa kuanza rasmi shughuli zake Februari, 11 2026.


