Na Mwandishi wetu, Katavi
MKUU wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, amesema utekelezaji wa Mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) katika Mji wa Mpanda utaleta mabadiliko chanya kwa wananchi na wageni katika utoaji huduma na mahitaji mbalimbali ya usafiri na usafirishaji, mazingira bora ya shughuli za kiuchumi na ongezeko la mapato kwa Halmashauri.
Mrindoko ameitaka Halmashauri ya Manispaa kufanya tathmini ya miradi yenye kujiendesha ihakikishe inaboresha huduma kuwa rafiki zaidi kwa wote pamoja na kuongeza mapato kwa Halmashauri na Serikali kwa ujumla.

Rai hiyo ameitoa Oktoba 25, 2025, wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba ya ujenzi wa miundombinu kupitia Mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC), wenye thamani ya Sh. bilioni 21.9, ambao utajumuisha ujenzi wa barabara 10 kwa kiwango cha lami, ujenzi wa jengo la usimamizi wa mradi na ununuzi magari manne ya kusimamia utekelezaji wa mradi.
“Natoa rai kwa Mkandarasi kuhakikisha kazi hizi zinafanyika kwa haraka, ubora uliokusudiwa na kukamilika kwa wakati kwa mujibu wa mkataba na mpango kazi uliokubalika ili wananchi waanze kunufaika na miundombinu hii ambayo Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza katika Manispaa yetu. Jukumu letu ni kuitunza miundombinu hii itakayojengwa kwa gharama kubwa ili iweze kudumu kwa muda mrefu.,” amesisitiza Mrindoko.
Pia amemtaka mkurugenzi wa Halmashauri kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mradi huo kwa kutumia rasilimali watu na vifaa vilivyopo kwenye Halmashauri.

“Niwatake pia Meneja wa TARURA (Mkoa na Wilaya) mshirikiane kwa karibu na ofisi ya mkurugenzi kwa kuzingatia muundo wa utekelezaji wa mradi huu wa TACTIC ambao unajumuisha wataalam kutoka pande zote mbili, alielekeza Mhe. Mrindoko.
Aidha, alieleza kuwa Manispaa ya Mpanda nayo imeingia katika kumbukumbu ya kuanza utekelezaji wa mradi baada ya kusaini mkataba kufuatia kukamilika kwa tathmini ya zabuni kwa mujibu wa taratibu za manunuzi ya umma.
Mkataba wa mradi wa TACTIC kwa Manispaa ya Mpanda unahusisha Uboreshaji wa Miundombinu ya Barabara za Mjini kati pamoja na Jengo la Usimamizi ambao utagharimu Sh. bilioni 21.9 bila kodi ya ongezeko la thamani (VAT).
Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda na Mkandarasi M/s Chonqing International Construction Corporation (CICO), wametiliana saini ya mkataba wa ujenzi wa barabara za kiwango cha lami zenye urefu wa Kilomita 8.4.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) Mratibu Msaidizi wa Mradi wa TACTIC, Mhandisi Emmanuel Manyanga, amesema utatekelezwa kwa miezi 15 kuanzia Novemba Mosi, 2025.

Mradi wa TACTIC ni mojawapo ya miradi inayofadhiliwa na Serikali kuu kupitia mkopo wa Benki ya Dunia wenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 410 (Bila VAT).
Mhandisi Manyanga amesema kuwa malengo ya mradi huo ni kuboresha miundombinu ya Miji 45 ya Tanzania pamoja na kujengea uwezo wa taasisi (Halmashauri) ili ziweze kujiimarisha katika usimamizi wa uendelezaji miji pamoja na ukusanyaji wa mapato.
Lengo kuu la mradi wa TACTIC ni kuboresha usimamizi wa ukuaji wa miji pamoja na kuziwezesha Halmashauri za Miji na Majiji kutoa huduma bora kwa wananchi.


