Mradi wa Taza kufungua Soko jipya la biashara ya umeme Afrika

Na Mwandishi Wetu, Mbeya

IMEELEZWA kuwa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Zambia kupitia Tunduma (TAZA) umefikia asilimia 83.45 huku ukitarajiwa kukamilika ifikapo Mei 2026 na hivyo kufungua soko jipya la biashara ya umeme barani Afrika.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huo leo Oktoba 23, 2025 katika eneo la Iganjo, Mbeya, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio amesema mradi wa TAZA ni muhimu kwa Taifa kwa kuwa utaiunganisha Tanzania na Nchi za ukanda wa Kusini mwa Afrika (Southern Africa Power Pool) na pia kuimarisha muunganiko wa ukanda wa Mashariki mwa Afrika (East Africa Power Pool).

“Nimshukuru na kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya nishati. Kupitia mradi huu tutaimarisha biashara ya kuuza na kununua umeme kati ya nchi za Mashariki mwa Afrika na zile zilizopo Kusini mwa Afrika”. Amesema Dkt. Mataragio.

Kuhusu biashara ya umeme ya kikanda, Dkt. Mataragio amesema kuwa tayari Tanzania imeshaunganisha gridi ya umeme na Nchi za Afrika za Kenya, Rwanda, Burundi na Ethiopia kupitia muunganiko wa East Africa Power Pool.

“Tutaunganisha pia gridi na nchi za Kaskazini na Magharibi mwa Afrika ili Afrika nzima tuweze kuuziana umeme ikiwa ni sehemu pia ya kutekeleza Mpango wa Nishati unaolenga kuwafikishia umeme waafrika takribani milioni 600 ambao bado hawajafikiwa na nishati ya umeme”. Amesisitiza Dkt. Mataragio

Kuhusu mradi wa TAZA, ameeleza kuwa unatekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ambao ni Benki ya Dunia, Umoja wa Ulaya na Shirika la Maendeleo la Ufaransa kwa Dola za kimarekani milioni 584.

Amesema kuwa mbali ya mradi wa TAZA kuunganisha gridi za umeme za Nchi za Kusini mwa Afrika, utauunganisha Mkoa wa Rukwa na umeme wa gridi pamoja na kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme katika Mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe.

Baada ya kukagua mradi huo, Dkt. Mataragio ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha linamsimamia Mkandarasi kwa karibu hasa katika kipindi hiki cha mvua ili hatua za awali za ujenzi wa misingi (foundation) ziweze kukamilika kwa wakati na kumtaka Mkandarasi kuhakikisha vifaa vyote vipo eneo la Mradi.

Katika hatua nyingine Dkt. Mataragio ameiagiza TANESCO kuhakikisha inapeleka umeme eneo la Ngozi unapotekelezwa mradi wa kuzalisha umeme kwa jotoardhi ambapo kwa hivi sasa mitambo ya uhakiki wa jotoardhi katika eneo hilo inatumia mafuta ya dizeli.

Katika ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu aliambatana na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Mha. Innocent Luoga na watendaji wa Wizara ya Nishati na TANESCO.

spot_img

Latest articles

Maaskofu, Masheikh nyanda za juu wahimiza uchaguzi wa amani

Na Mwandishi Wetu, Mbeya VIONGOZI wa dini kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wamewataka...

SGR yapata ajali, TRC yataja chanzo

Na Mwandishi Wetu Treni ya Mwendokasi (SGR) imeacha njia yake na kupata ajali katika eneo...

Yajayo baada ya uchaguzi mkuu yahitaji hekima kubwa

JUMATANO ijayo, OKTOBA 29, 2025, taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linakwenda kuongeza...

More like this

Maaskofu, Masheikh nyanda za juu wahimiza uchaguzi wa amani

Na Mwandishi Wetu, Mbeya VIONGOZI wa dini kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wamewataka...

SGR yapata ajali, TRC yataja chanzo

Na Mwandishi Wetu Treni ya Mwendokasi (SGR) imeacha njia yake na kupata ajali katika eneo...