Na Mwandishi Wetu
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)Tanzania Bara, John Heche, amekamatwa na Polisi wakati akiingia Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam na kusafirishwa kwenda Tarime.
Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika amesema kiongozi huyo alikuwa anakwenda mahakamani kwa ajili ya kusikiliza kesi ya Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu inayoendelea.
Akizungumzia sababu za kukamatwa kwa Heche, mbeleza na waandishi wa habari leo Oktoba 22,2025, Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa Chadema, Wakili Gaston Garubindi amesema wamefuatilia na kuambiwa na Jeshi la Polisi kuwa jambo la Heche halipo Dar es Salaam lipo Tarime na wamedai kuwa tayari wameshamsafirisha kuelekea huko.

“Taarifa ya Jeshi la Polisi wanadai ni kweli wamemkamata John Heche, kwa makossa ambayo hawajayasema, lakini anasema jambo lake lipo Tarime na kwamba tuhuma zake zipo kule na tayari wamemsafirisha kutoka Dar es Salaam kwenda Tarime.
“Kama Chama tunajipanga sasa kwa maana ya kuagiza mawakili waliopo Mkoa wa Mara na wengine kutoka Mwanza ili waelekee huko ili kutoa huduma ya Kisheria kwa Makamu Mwenyekiti,” amesema Wakili Garubindi.
Amesema Heche alikuwa hajapewa wito wowote wa kuitwa Polisi, hivyo wanasubiria atakapofikishwa hule watajua tuhuma zake ni nini.