Na Mwandishi Wetu
Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Matha Japheth (44), kabila ni Mnyamwezi , Mkulima Mkazi wa Kitongoji cha Mzalendo Kijiji cha Mawemeru , Kata ya Nyarugusu Wilaya ya Geita kwa tuhuma za kumuuwa mume wake na kumfukia katika shimo ndani nyumba yao.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo taarifa ya awali inaeleza chanzo ni mgogoro wa kifamilia baina ya mke na mume ambaye kwa sasa ni marehemu.
“Baada ya mahojiano makali mwanamke huyu alikiri kwamba marehemu ni mume wake na kwamba siku hiyo ya tarehe 11 majira ya usiku mwanaume alirudi nyumbani lakini wakawa na ugomvi ambao ulisababisha kumshambulia kwa kitu chenye ncha kali na baada ya kumshambulia mwanaume huyo alifariki dunia na baada ya hapo akaamua kuchimba shimo ndani ya nyumba yao na kisha kumfukia,“ amesema Kamanda Safia.

