Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza mafanikio ya makusanyo ya mapato kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026, baada ya kufanikisha kukusanya jumla ya Sh. Trilioni 8.97, sawa na ufanisi wa asilimia 106.3 ya lengo lililokuwa Sh. Trilioni 8.44.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Oktoba 2, 2025 na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, imeeleza kuwa makusanyo hayo yameonyesha ongezeko la asilimia 15.1 ikilinganishwa na Sh. Trilioni 7.79 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita wa fedha 2024/2025.
“Makusanyo haya pia ni sawa na ukuaji wa asilimia 104 ukilinganisha na Sh. Trilioni 4.40 zilizokusanywa katika kipindi kama hiki kuanzia Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ilipoingia madarakani mwaka wa fedha 2020/2021,” amesema Mwenda.
Ameongeza kuwa wastani wa makusanyo ya kila mwezi umeongezeka kutoka Sh. Trilioni 1.47 mwaka 2021/2022 hadi Sh. Trilioni 2.99 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
“Kwa mara ya kwanza, TRA imeweza kukusanya kiasi cha Sh. Trilioni 3.47 katika mwezi mmoja wa Septemba 2025, rekodi ambayo haijawahi kufikiwa nyuma,” amesema.
Amebainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na kuendelea kuboresha mahusiano na walipakodi, utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia ya kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari bila uonevu, pamoja na uboreshaji wa mazingira ya biashara.
“Kuongezeka kwa uwajibikaji wa ulipaji kodi wa hiari, ukuaji wa shughuli za kiuchumi, sera bora za kiuchumi na uanzishwaji wa Dawati la Uwezeshaji Biashara nchi nzima vimekuwa chachu kubwa ya mafanikio haya,” ameongeza Mwenda.
Aidha, TRA imesema kuwa muitikio mzuri wa wafanyabiashara wa mtandaoni, hasa katika sekta ya huduma za malazi, umesaidia kuongeza makusanyo.
“Vilevile, kuimarisha usimamizi wa vyanzo vya Forodha kupitia mfumo wa TANCIS ulioboreshwa na kuongeza ufanisi katika uondoshaji mizigo kwenye vituo vya Forodha kumesaidia kuvuka malengo,” amesema.
Mwenda amewashukuru walipakodi wote kwa uwajibikaji wao, na kuahidi TRA itaendelea kusimamia nidhamu, ubunifu na mafunzo ya watumishi wake ili kuhakikisha mapato yanaendelea kuongezeka kwa maendeleo ya Taifa.