Jamii yatakiwa kupaza sauti kukomesha ukatili wa kijinsia

Na Tatu Mohamed

JAMII imetakiwa kuendelea kupaza sauti kwa pamoja ili kutokomeza ukatili wa kijinsia unaoendelea kushamiri katika maeneo mbalimbali nchini, hususan miongoni mwa watoto, wanawake na makundi mengine yaliyo katika mazingira magumu.

Wito huo umetolewa jana na Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Dkt. Rose Reuben, wakati wa mafunzo yaliyofanyika chini ya mradi uitwao ‘Sauti Zetu’ unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya TAMWA na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).

Alisema ukatili wa kijinsia umeendelea kuwa tatizo sugu katika jamii, na matukio yake yamekuwa yakiongezeka mara kwa mara hata katika maeneo ya wazi.

Amefafanua kuwa, ukatili wa kisaikolojia unaonekana kuwa mkubwa zaidi, kwani mtu anapoumizwa kisaikolojia anaweza kuwa chanzo cha ukatili mwingine katika jamii.

“TAMWA peke yake haiwezi kukomesha tatizo hilo bila ushirikiano kutoka kwa jamii, serikali na wadau mbalimbali hivyo ni lazima jamii nzima ishiriki kupaza sauti ili kuleta suluhisho la kweli kwa janga hili la ukatili wa kijinsia,” alisisitiza.

Akizungumzia kuhusu mafunzo hayo, Dkt. Rose alisema yamelenga kuiwezesha jamii kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu ukatili wa kijinsia na kupaza sauti dhidi ya vitendo hivyo.

“Tumejumuisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, kina mama kutoka masokoni, maafisa wa serikali kutoka ngazi mbalimbali, na waandishi wa habari kwa lengo la kujadili namna bora ya kukomesha ukatili huu,” alisema Dkt. Reuben.

Maoni ya washiriki

Akizungumza katika mafunzo hayo, Mwalimu Annamaria Ngawambala wa Shule ya Sekondari Mugabe alisema kuwa ukatili wa kijinsia kwa watoto bado ni changamoto kubwa, hasa kwa familia zenye hali duni ya kiuchumi.

“Mtoto anakosa mahitaji ya msingi, haendi shule na hujikuta akijihusisha na shughuli zisizofaa kwa umri wake. Utengano wa wazazi huathiri malezi, huku walimu wakibeba mzigo mkubwa wa kulea watoto pekee yao,” alisema Mwalimu Ngawambala.

Kwa upande mwingine, kina mama wa masokoni walieleza kuwa hukumbana na ukatili wa aina mbalimbali ikiwemo lugha za matusi kutoka kwa wateja au wenza wao.

Mkurugenzi wa Taasisi ya WAJIKI, Janeth Mawinza, alisema taasisi hiyo inashughulika na chanzo cha ukatili wa kingono kwa lengo la kuzuia vitendo hivyo.

Ameeleza kuwa wameanzisha kampeni ya Safari Salama bila rushwa ya ngono kwa wasichana, ambapo wanatembelea shule mbalimbali na vituo vya bodaboda kutoa elimu kwa wanafunzi na vijana.

Kwa upande wake, Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka Kituo cha Mkono kwa Mkono Mwananyamala, Halili Katani, alisema kuwa serikali inaendelea kulishughulikia tatizo hilo kwa nguvu zote ili kuhakikisha kuwa wahanga wanapata huduma stahiki kwa wakati.

“Wahanga wa ukatili wanapaswa kupata huduma kutoka kwa polisi, wahudumu wa afya, maofisa ustawi na watoa huduma wengine mahali pamoja,” alisema Katani.

Baadhi ya wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo walieleza aina ya ukatili wanaokutana nao, kama vile lugha za matusi kutoka kwa makonda wa daladala na kejeli kutoka kwa walimu wawapo shuleni.

“Unakuta unataka kupanda daladala, konda anakusukuma au hakurudishii chenji. Shuleni, ukikosea kujibu swali, mwalimu anakutukana na wenzako wanakucheka,” alisema mmoja wa wanafunzi hao.

Mhariri Mtendaji wa Uhai FM, Frank Sanga, akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, alitaja sababu mbalimbali za ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na matatizo ya afya ya akili, migogoro ya kifamilia, umasikini, na jamii kumsahau Mungu.

spot_img

Latest articles

TRA yakusanya Trilioni 8.97 kwa robo ya kwanza, yazidi lengo kwa asilimia 106.3

Na Mwandishi Wetu  MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza mafanikio ya makusanyo ya mapato kwa...

Rais Samia awapiga chini mabosi Mwendokasi

Na Mwandishi Wetu, The Media Brains Rais Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa mabosi wapya...

Kiti Baraza la Usalama kitaondoa maafa Afrika?

MKUTANO Mkuu wa Baraza la Umoja wa Mataifa wa 80 ulimalizika jijini New York,...

Bei za Petroli, Dizeli zaendelea kushuka

Na Mwandishi Wetu BEI ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa...

More like this

TRA yakusanya Trilioni 8.97 kwa robo ya kwanza, yazidi lengo kwa asilimia 106.3

Na Mwandishi Wetu  MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza mafanikio ya makusanyo ya mapato kwa...

Rais Samia awapiga chini mabosi Mwendokasi

Na Mwandishi Wetu, The Media Brains Rais Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa mabosi wapya...

Kiti Baraza la Usalama kitaondoa maafa Afrika?

MKUTANO Mkuu wa Baraza la Umoja wa Mataifa wa 80 ulimalizika jijini New York,...