Na Tatu Mohamed
MWANAFUNZI wa Shahada ya Kompyuta Sayansi kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Wandowa Titus, amebuni mfumo wa kiteknolojia unaotumia Akili Mnemba (AI) kuhesabu idadi ya abiria katika vituo vya mabasi yaendayo haraka (Mwendokasi).
Akizungumza leo Septemba 24, 2025 jijini Dar es Salaam katika Kongamano la Wahandisi Vijana, Wandowa amesema mfumo huo umetengenezwa mahsusi kusaidia kutatua changamoto ya msongamano mkubwa wa abiria kwenye vituo vya Mwendokasi na kuwezesha usimamizi bora wa usafiri huo wa umma.
“Mfumo huu utakuwa na kamera maalumu zitakazowekwa kwenye vituo vya kusubiri mabasi, ambapo zitahesabu idadi ya watu waliopo na kueleza wanaoelekea maeneo tofauti kama vile Kimara, Mbezi, Gerezani na Morocco. Hii itawasaidia wasimamizi kujua abiria wangapi wanahitaji huduma kwa wakati fulani na kupeleka mabasi kwa haraka,” amesema.

Ameeleza kuwa wazo hilo lilimjia kutokana na hali ya msongamano mkubwa katika vituo, hali ambayo husababisha kero mbalimbali ikiwemo ucheleweshaji wa huduma na vitendo vya wizi.
“Niliona kuna ulazima wa kuja na suluhu itakayosaidia kupunguza usumbufu kwa abiria na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mabasi ya Mwendokasi,” amesema Wandowa.
Kwa mujibu wake, mfumo huo ukipewa nafasi ya kuendelezwa na kuungwa mkono na mamlaka husika, unaweza kuboresha huduma ya usafiri wa umma jijini Dar es Salaam na kuondoa malalamiko ya abiria kuhusu ucheleweshaji na msongamano kwenye vituo.

Naye Mhitimu wa Shahada ya Uhandisi wa Matengenezo ya Ndege kutoka NIT, Ladislaus Moshi amebuni na kutengeneza mfumo utakaosaidia kutambua vitu hatarishi vilivyopo kwenye njia ya kutua na kupaa kwa ndege.
Moshi amesema mfumo huo unaweza kutoa taarifa mapema na kwa haraka kwa wasimamizi wa viwanja vya Ndege nchini juu ya aina yoyote ya taka au kihatarishi kilichopo kwenye njia ya kutua na kupaa kwa ndege.

Amesema kwa sasa ukaguzi wa njia hizo unafanywa na kikosi maalum cha Zimamoto ambao wamekuwa wakitembea katika njia hiyo asubuhi na jioni ili kutoa vihatarishi vilivyopo vinavyoweza kuleta madhara pindi ndege inapotaka kutua au kupaa.
Moshi amesema njia hiyo inayotumika sasa inaleta hasara kwa Taifa kwani inabidi ndege zinapotaka kutua au kupaa zisubiri ukaguzi huo hali inayochangia abiria kuchelewa kuondoka au kutua na hivyo kupoteza mapato.

“Mfumo huu ukitumika utaongeza ufanisi, utakuza mapato kwa sababu utatoa taarifa mapema na kwa haraka juu ya kitu hatarishi kilichopo katika njia ya kutua ndege na hakuna kusubiri, vitu hivi hatarishi tunavyosema vinaweza kuwa chupa, tairi au hata ndege yenyewe,” amesema.
Aidha ametoa wito kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kuutumia mfumo huo ili kuweza kuongeza mapato ya nchi.