PBA yapinga uamuzi wa TLS kuzuia msaada wa kisheria kwa wananchi

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Mawakili wa Serikali (PBA) kimepinga vikali hatua ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kutoa maelekezo yanayozuia wanasheria kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi, kufuatia tukio la kushambuliwa kwa Wakili Deogratius Mahinyila na askari polisi Septemba 15, 2025, alipokuwa akifuatilia kesi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Septemba 23, 2025, Mwenyekiti wa PBA, Addo Mwasongwe, amesema kutokana na matamko na maazimio mbalimbali yaliyotolewa na TLS yaliyolenga kuzuia mawakili kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi ni kinyume na misingi ya taluma ya uwakili na pia ni uvunjaji wa haki za kikatiba za wananchi kupata msaada huyo.

“Jukumu mojawapo la wakili ni lazima uwe unatoa msaada wa kisheria, kuna watu wenye uwezo na kuna watu wasio na uwezo. Kwa wasio na uwezo tumelazimishwa na sheria kwamba ni lazima kuwahudumia na sio suala la maamuzi yetu sisi” amesema Mwasongwe.

Ameeleza kuwa TLS haina mamlaka yoyote ya kuzuia misaada ya kisheria, na kwamba hatua hiyo inahatarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi wa kawaida.

“Kitendo cha TLS kinavuruga mfumo wa utoaji haki na kinawanyima wananchi haki yao ya kikatiba,” amesisitiza.

Mwasongwe amesema nidhamu ya wakili ipo chini ya Kamati ya nidhamu ya mawakili kwa mujibu wa Advocate Act na si jukumu la baraza la TLS pekee.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 13 cha Advocate Act (Cap.341) nidhamu ya mawakili ipo chini ya Kamati ya nidhamu ya mawakili (Advocates Disciplinary Committee) inayoundwa na Jaji wa Mahakama Kuu (Mwenyekiti),Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Mwanachama mmoja wa TLS.

Hii inamaanisha kuwa nidhamu ya wakili si jukumu la TLS pekee bali ni jukumu la pamoja chini ya mahakama. Hivyo ni wajibu wa Kamati ya Nidhamu kuchunguza kauli au vitendo vinavyoweza kuashiria uvunjifu wa sheria au ukiukaji wa maadili ya kitaaluma,”amesema.

Amesema TLS ni chama cha kitaaluma chenye wajibu wa kuhakikisha weledi,ubora na heshima ya taaluma ya uwakili unadumishwa kwa mujibu wa TLS Act.

“Tunashauri kwa heshima ya viongozi wa TLS kuzingatia wajibu wao wa kisheria na kitaaluma na kuepuka maamuzi yanayoweza kuathiri haki za wananchi na heshima ya taaluma ya uwakili.” alisema.Mwasongwe amesema sheria Legal Aid Act(Cap.21 R.E 2019) inatamka wazi utoaji wa msaada wa kisheria ni jukumu la kisheria si tendo la hiari.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 5(1),Serikali na taasisi zilizosajiliwa zinzwajibu wa kuhakikisha upatikanaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi.‘Kifungu cha 6 na 7 cha sheria hiyo kimeipa TLS jukumu mahsusi la kuratibu na kutoa msaada wa kisheria kupitia wanachama wake,” amesema.

Ameongeza kuwa utoaji wa huduma za kisheria kwa wananchi zimekusudiwa kwa wananchi wa kipato cha chini na makundi maalum yasiyoweza kumudu gharama za uwakili.

Amesema TLS kama taasisi ya kisheria inawajibu wa kikatiba wa kuhakikisha kwamba maamuzi yake hayapingani na sheria iliyoianzisha (TLS Act)na sheria nyingine husika kama Legal Aid Act.

“Katika ibara ya 26 (1) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 inasema kila mtu anawajibu wa kutoo katiba na sheria za Jamhuri ya Muungano.

“Huku katika ibara ya 13(1)ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 inasema watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki sawa bila ya ubaguzi wowote,hivyo kuwanyima wananchi wa kipato cha chini msaada wa kisheria kitendo cha ubaguzi (Discrimination) kinachopingana na Katiba ,kwa kuwa kinawanyima haki sawa ya kupata huduma za kisheria,” alisisitiza.

Baadhi ya Wanachama TLS wafunguka

Wakili wa Kujitegemea, Diana Rwegasira amesema tamko lililotolewa na TLS sio zuri kwani TLS ni chama cha kisheria na taasisi ya kisheria na jicho la kisheria na ipo nchini Kisheria lakini cha kushangaza imetoa maamuzi ambapo hayapo kisheria.

Amesema suala la huduma za kisheria kusimamishwa si haki na si sawa kwa sababu ipo kinyume na sheria TLS ni taasisi mojawapo ya kisheria ambayo inajukumu ya kuhakikisha kwamba huduma hizo za kisheria inatolewa kwa wananchi.

“Jukumu la kutolewa huduma za kisheria sio la hiari ni matakwa ya kisheria ni kitu cha ajabu na cha kusikitisha na kuona kwamba wao TLS wapo kisheria na wanafanya kazi kisheria alafu wanakinzana na sheria,” amesema.

Rais Mstaafu TLS Wakili wa Kujitegemea,Francis Stolla, amesema maazimio kumi yaliyotolewa yalikuwa mazuri isipokuwa maazimio mawili hayaendani kisheria ikiwemo azimio la Wito wa Baraza la Viongozi kuwazuia wanachama wake mawakili na wanasheria wasijiusishe katika kutoa msaada wa sheria.

Amesema azimio hilo linahitilafu kwasababu linalenga wanachama wasitekeleze sheria Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ametoa wito kwa TLS, ni vizuri kutetea haki za wanachama wake wanaoingia katika migogoro wakati wakifanya kazi zao za kutekeleza sheria,lakini Chama kisiwaingize wanachama wake katika mgogoro na sheria na kufanya wakiuke haki ya kuwasaidia wananchi.

spot_img

Latest articles

Mwanamke ashikiliwa  Polisi kwa  kumuua mume wake na kumfukia ndani ya nyumba yao

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina...

Padre aliyepotea apatikana akiwa hai

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma limefanikiwa kumpata Padre Camillus Nikata wa Jimbo...

Waangalizi wa Uchaguzi watakiwa kutoingilia mchakato wa Uchaguzi Mkuu

Na Mwandishi wetu, Dodoma WAANGALIZI wa Uchaguzi wa ndani na wa kimataifa wametakiwa kuzingatia sheria...

More like this

Mwanamke ashikiliwa  Polisi kwa  kumuua mume wake na kumfukia ndani ya nyumba yao

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina...

Padre aliyepotea apatikana akiwa hai

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma limefanikiwa kumpata Padre Camillus Nikata wa Jimbo...

Waangalizi wa Uchaguzi watakiwa kutoingilia mchakato wa Uchaguzi Mkuu

Na Mwandishi wetu, Dodoma WAANGALIZI wa Uchaguzi wa ndani na wa kimataifa wametakiwa kuzingatia sheria...