Na Mwandishi Wetu
Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga na Mloganzila),imetoa ufafanuzi kuhusu utaratibu wa uchangiaji figo kwa wagonjwa wanaohitaji huduma ya kupandikiza viungo hivyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Septemba 2, na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha, huduma za upandikizaji figo zilianza kutolewa rasmi Septemba 2017 na hadi sasa wagonjwa 106 wameshanufaika.
Aligaesha amesema hospitali inazingatia Kanuni za Huduma za Figo zilizotungwa mwaka 2017 kwa kuendana na miongozo na maazimio ya Kimataifa yaliyoidhinishwa na Wizara ya Afya, ambayo yanakataza biashara ya uuzaji viungo vya binadamu.
Aidha, ameeleza kuwa ndugu wa karibu wa mgonjwa pekee ndiye anayeruhusiwa kuchangia figo na uchangiaji huo hufanyika bila malipo.
Ameongeza kuwa kuna Kamati Maalumu ya Uidhinishaji inayojumuisha wanasheria, viongozi wa dini, madaktari na maafisa ustawi wa jamii, ambayo hupitia maombi yote ya upandikizaji figo.
Kamati hiyo hukagua nyaraka za uthibitisho wa uhusiano wa damu kati ya mgonjwa na mchangiaji, ikiwamo viapo, vyeti vya kuzaliwa, picha pamoja na majibu ya vipimo vya maabara.
Hata hivyo Hospitali ya Taifa Muhimbili imesisitiza kuwa itaendelea kuhakikisha huduma ya upandikizaji figo inatolewa kwa mujibu wa kanuni zake na miongozo ya kimataifa.