Na Tatu Mohamed
VYAMA vya siasa nchini vimetakiwa kuhakikisha wagombea wao wanazingatia matakwa ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 (Sura ya 278), ili kudhibiti matumizi ya fedha zisizo halali na kulinda usawa wa kidemokrasia katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Hayo yameelezwa leo Agosti 18, 2025 jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Sehemu ya Ruzuku kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, CPA Edmund Mugasha kwenye Mafunzo kuhusu Sheria ya Gharama za Uchaguzi kwa viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa.
Amesema Sheria hiyo inaweka sharti la kila chama na kila mgombea kuweka wazi mapato na matumizi ya gharama za uchaguzi, jambo ambalo ni msingi wa uchaguzi huru na wa haki.

“Kila chama na mgombea anatakiwa kutangaza mapato na matumizi ya kampeni. Viongozi mna jukumu la kuhimiza wagombea wenu kutekeleza hili kwa uwazi,” amesema Mugasha, akifafanua kuwa udhibiti wa gharama ni nyenzo muhimu ya kulinda demokrasia.
Awali, akifungua mafunzo hayo Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amewataka viongozi wa vyama vya siasa nchini kuhakikisha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025 zinafanyika kwa amani na kistaarabu, bila kutumia lugha za matusi, kashfa au vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha mshikamano wa taifa.
Amesema vyama vina wajibu wa kuendeleza misingi ya amani na mshikamano uliorithiwa kutoka kwa waasisi wa taifa.
“Nendeni mkafanye kampeni za kistaarabu mkiwanadi wagombea wenu. Jiepusheni kabisa na lugha za matusi, kashfa, uchochezi au vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga amani na utulivu wa taifa letu,” amesema Jaji Mutungi.
Amesisitiza kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi na kwamba siasa hazipaswi kugeuzwa chanzo cha migawanyiko.
“Uchaguzi si mwisho wa siasa wala maendeleo. Turithishe amani hii kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo,” ameongeza.
Aidha, Msajili amewataka viongozi wa kisiasa kutochukulia kwa uzito taarifa za upotoshaji zinazosambazwa kupitia mitandao ya kijamii, akieleza kuwa uchaguzi utafanyika kama ulivyopangwa.
“Mtaambiwa uchaguzi haupo, msikate tamaa. Uchaguzi upo, na jambo kubwa zaidi ni kuhakikisha tunaingia kwenye uchaguzi huru na wa haki kwani ninyi ndio wakala wa kwanza wa kuhakikisha hilo linatekelezeka,” amehimiza.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Khatibu, alikumbusha historia ya changamoto zilizojitokeza mwaka 2010 wakati sheria hiyo ilipoanza kutumika, ambapo baadhi ya wagombea walijaza taarifa za uongo na risiti za kughushi.
“Changamoto hizo zilionekana kwa sababu ya uelewa mdogo, lakini leo tunatarajia kupata elimu ya kutosha ili kuhakikisha kasoro hizo hazijirudii,” amesema Khatibu.