Na Tatu Mohamed, Dodoma
CHUO cha VETA Kihonda kimebuni mashine mpya ya kusaga chumvi ya mawe, hatua inayolenga kuongeza thamani ya zao hilo na kurahisisha matumizi yake katika sekta mbalimbali.
Akizungumza kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma, Mkufunzi Mwandamizi wa chuo hicho, Fredrick Uliki, amesema mashine hiyo imeundwa mahsusi kwa ajili ya kusaidia wakulima wadogo wa chumvi hususani wa Bagamoyo na Lindi ambao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kusaga chumvi.

“Chumvi inapokuwa unga, matumizi yake yanapanuka zaidi. Kwa mfano, kwenye nyama ya kuchoma au chakula cha mifugo, ni lazima utumie chumvi ya unga. Pia, chumvi ikisagwa ni rahisi kuongeza madini joto na virutubishi vingine,” amesema Uliki.
Amefafanua kuwa, Mashine hiyo ina uwezo wa kusaga kilo 100 hadi 150 kwa saa, na imetengenezwa kwa malighafi imara zisizoshika kutu, jambo linaloifanya idumu kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa Uliki, teknolojia hiyo inalenga kusaidia wakulima kuongeza thamani ya chumvi yao, kuisafirisha kwa urahisi zaidi na kupata soko pana.