Na Mwandishi Wetu
CHUO cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kimeendelea kuonyesha ubora wake baada ya kushinda mashindano ya The Tanzania Institute of Bankers (TIOB) Scholar Banking Challenge kwa mfululizo wa miaka miwili, ambapo mwaka huu pia kimeongoza miongoni mwa vyuo vikuu zaidi ya 50 vilivyoshiriki.
Hayo yalisemwa juzi na Grace Kazoba, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko cha IFM, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya chuo hicho katika mashindano hayo.
Kazoba alibainisha kuwa kati ya wanafunzi 3,500 waliojitokeza kushindana, IFM imeonyesha ushindi mkubwa kwa kuwa na wanafunzi tisa bora wa kwanza kutoka chuo hicho.

“Wanafunzi wetu walishiriki kwa ushindani mkubwa na kufanya vizuri hadi kutwaa nafasi za juu zaidi,” alisema.
Aidha, alifafanua kuwa mwaka jana, wanafunzi wa IFM wa Shahada ya Sayansi katika Uchumi na Fedha (BEF) walishiriki katika mashindano ya Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) 2024, ambapo walionyesha jinsi ya kutengeneza faida kubwa kupitia ushiriki wa soko la hisa.
“Mwanafunzi anaamka asubuhi akifuatilia kampuni zinazofanya vizuri, na kwa kufanya hivyo kwa muda mrefu, wengi wetu walifanikiwa,” aliongeza Kazoba.
Alisema pia kuwa katika orodha ya sifa bora 30, wanafunzi wengi walitoka IFM, ambapo walionyesha uhalisia wa hali halisi wa soko la hisa na kupata tuzo kwa juhudi zao.
Ushindi huu unaonesha IFM kuendelea kuwa chuo kinachotoa elimu bora katika fani za fedha na uchumi, na kuhimiza wanafunzi wake kushindana kitaalamu na kufanikisha malengo yao katika sekta ya fedha nchini.