Na Tatu Mohamed
MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri, ametembelea banda la Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) katika Maonesho ya Wakulima ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, ambapo ametoa wito kwa taasisi hiyo kushirikiana na vyama vya waendesha bodaboda na taasisi nyingine ili kutoa elimu ya usalama barabarani kwa jamii.

Akizungumza leo Agosti 6, 2025, Shekimweri ameipongeza MOI kwa kazi kubwa ya kutoa huduma za kibingwa kwa wahanga wa ajali, huku akiitaka taasisi hiyo kushiriki kikamilifu katika kampeni za kuzuia ajali za barabarani kwa kushirikiana na wadau kama VETA na vyama vya bodaboda, yakiwemo UWAMIDO na vinginevyo.
“Nawapongeza MOI kwa kazi nzuri mnayofanya. Lakini nawasihi mshirikiane na taasisi kama VETA na vyama vya bodaboda kama UWAMIDO ili kuwafikia waendesha bodaboda wengi zaidi kwa elimu ya usalama barabarani. Hii itasaidia kupunguza ajali na ulemavu unaotokana na uzembe au kutozingatia sheria,” amesema Shekimweri.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ametoa pendekezo la kufanyika kwa ziara maalum kwa waendesha bodaboda kutembelea majeruhi waliolazwa MOI kutokana na ajali, ili kujifunza kwa vitendo madhara ya ajali na hivyo kuchukua tahadhari.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Radiolojia kutoka MOI, Dkt. Angela Isangya, amesema taasisi hiyo iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa elimu ya kinga na usalama barabarani ili kupunguza ajali na ulemavu unaoweza kuzuilika.

Maonesho hayo ya Nanenane ambayo yameanza rasmi Agosti 1, 2025, yanatarajiwa kufikia tamati Agosti 8, 2025, yakiwa na kaulimbiu isemayo: “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025.”