Na Tatu Mohamed
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imesema imeweka mazingira wezeshi kuhakikisha makundi maalum wakiweko watu wenye ulemavu wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi Mkuu kwani kila Mtanzania ana haki ya kuchagua viongozi wake bila kizuizi chochote.
Hayo yamebainishwa leo Julai 31, 2025 na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele wakati akifungua mkutano kati ya Tume na wawakilishi wa watu wenye ulemavu.

“Tunaendelea kuboresha mazingira ili kuhakikisha kila mtu, wakiwemo watu wenye ulemavu, anashiriki uchaguzi kwa heshima, usawa na faragha. Tume tayari imeandaa karatasi za kura zenye maandishi ya nukta nundu kwa wapiga kura wasioona, pamoja na vituturi maalum kwa wenye ulemavu wa viungo,” amesema Jaji Mwambegele.
Amefafanua kuwa, watu wenye ulemavu wana nafasi ya kipekee katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kushiriki uchaguzi na kwamba Tume inathamini sana ushirikiano wao katika hatua mbalimbali za maandalizi.

Aidha, amewapongeza wawakilishi hao kwa ushirikiano mkubwa walioutoa wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, hatua ambayo ni muhimu kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Akielezea kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo, Jaji Mwambegele amesema kuwa Tume imeshatangaza ratiba ya uchaguzi ambapo utoaji wa fomu za uteuzi utaanza rasmi Agosti 9, 2025 huku kampeni zikipangwa kuanza Agosti 28 hadi Oktoba 28, 2025 kwa Tanzania Bara, na Oktoba 27 kwa upande wa Zanzibar.

Katika mkutano mwingine na wawakilishi wa wanawake, Makamu Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa Jaji wa Mahakama ya Rufani (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk, amewahimiza wanawake kutumia nafasi zao kuwafikishia wananchi taarifa sahihi kuhusu hatua za maandalizi ya Uchaguzi Mkuu, na kuhamasisha waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura.
Jaji Mbarouk ametoa pongezi kwa wanawake kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha katika kipindi chote cha uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kilichoanza tarehe 20 Julai 2024 na kukamilika tarehe 4 Julai 2025.
“Natoa pongezi kwenu kwa namna mlivyotuunga mkono wakati wote wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.Kwa upande wake, Mjumbe wa Tume, Mheshimiwa Jaji wa Mahakama Kuu Asina Omari, amewahimiza vijana kutumia mitandao ya kijamii kwa uadilifu, hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.

“Natoa wito kwenu kuwahamasisha vijana kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na kuepuka mitandao inayosambaza habari za chuki na uchochezi,” amesema Jaji Asina.
Ameonya pia dhidi ya matumizi mabaya ya teknolojia ya akiliunde (AI), ambayo kwa sasa inatumika kusambaza taarifa za upotoshaji na chuki.Katika mikutano yote hiyo, viongozi wa Tume wamekumbusha kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 utafanyika kwa mujibu wa sheria mbili mpya zilizopitishwa mwaka 2024, ambazo zimeleta maboresho ya kiutendaji, kisheria na kiuwazi katika mchakato mzima wa uchaguzi.
Kauli mbiu ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ni ‘Kura Yako Haki Yako, Jitokeze Kupiga Kura’.