Na Mwandishi Wetu
Watoto watano waliokuwa wanalelewa katika kituo cha watoto yatima cha Igambilo Manispaa ya Tabora, wamefariki dunia baada ya bweni walililokuwa wamelala kuteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo Julai 29,2025.
Katika tukio hilo, mbali ya watoto waliofariki, wengine sita wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kitete kwa ajili ya kupatiwa matibabu baada ya kupata majeraha ya moto.
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imesema imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya watoto hao watano, huku ikitoainatoa wito kwa Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu chanzo cha tukio hilo.
Katika taarifa ya wizara hiyo leo, Julai 29, 2025, imetoa inatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki tukio hilo la kusikitisha na kuwakumbusha wasimamizi na wamiliki wa makao yote ya watoto nchini kuhakikisha kuwa wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara wa mifumo ya umeme, pamoja na kuweka na kuimarisha miundombinu ya kinga dhidi ya majanga ya moto.
“Serikali inahakikisha majeruhi wanapata matibabu bure, watoto wengine wanapatiwa mahala salama pa kuishi na kupatiwa msaada wa kisaikolojia na kijamii kupitia maafisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri.
Pia Wizara itaendelea kufuatilia kwa karibu
mwenendo wa tukio hili na kuchukua hatua stahiki za kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto katika makao yote ya watoto nchini,” imesema taarifa hiyo ya Waziri wizara hiyo Dk. Dorothy Gwajima.