Na Tatu Mohamed
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ni taasisi ya serikali iliyo chini ya Wizara ya Afya yenye jukumu la kulinda afya ya jamii kwa kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa dawa pamoja na vifaa tiba vinavyotumika nchini.
Matumizi ya dawa kiholela yameendelea kuwa tatizo kubwa linalokumba sekta ya afya, hasa katika jamii ambako baadhi ya watu hujichukulia maamuzi ya kutumia dawa bila vipimo au ushauri wa kitaalamu.
Hali hii husababisha madhara makubwa ikiwemo kuibuka kwa usugu wa dawa, hasa za kuua bakteria (antibiotics), kuongezeka kwa gharama za matibabu, pamoja na hatari ya kupata madhara makubwa kiafya au kifo.

Aidha, matumizi yasiyo sahihi ya dawa yanaweza kuficha dalili za ugonjwa na kuchelewesha matibabu sahihi, jambo linaloweza kufanya hali ya mgonjwa kuwa mbaya zaidi.Ili kukabiliana na changamoto hiyo, TMDA imeweka mfumo madhubuti wa usajili wa dawa zote kabla hazijaruhusiwa kuingia sokoni.
Kila dawa hupitia uchunguzi wa kina wa kisayansi ili kuhakikisha kuwa inakidhi viwango vya ubora, usalama na ufanisi. Hatua hii husaidia kuzuia uwepo wa dawa duni au bandia ambazo zinaweza kuhatarisha maisha ya watumiaji.
Vilevile, mamlaka husajili na kukagua maeneo ya biashara ya dawa kama famasi na maduka ya dawa muhimu ili kuhakikisha kuwa dawa zinauzwa katika mazingira salama na kwa kufuata miongozo ya kitaalamu.

Sambamba na hilo, TMDA hudhibiti matangazo ya dawa ili kuzuia upotoshaji wa taarifa kwa umma kwani matangazo yasiyo sahihi yanaweza kuwashawishi wananchi kutumia dawa zisizofaa kwa hali zao za kiafya au kutumia dawa kwa dozi zisizo sahihi.
Kupitia udhibiti huu, mamlaka huhakikisha kuwa taarifa zinazotolewa kwa umma ni sahihi na zinazingatia misingi ya kitaalamu, hivyo kusaidia kupunguza matumizi ya dawa kiholela.
Katika kuimarisha udhibiti, TMDA pia hutekeleza mfumo wa ufuatiliaji wa dawa baada ya kuingia sokoni unaojulikana kama Post Marketing Surveillance (PMS) ambapo kupitia mfumo huu, sampuli za dawa hukusanywa kutoka maeneo mbalimbali na kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara ili kuthibitisha ubora wake.

Dawa zitakazobainika kuwa na dosari huondolewa sokoni mara moja. Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa hata baada ya kusajiliwa, dawa zinaendelea kuwa salama na zenye ufanisi kwa watumiaji.
Mbali na udhibiti wa bidhaa, TMDA imekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya dawa. Kupitia kampeni mbalimbali za uelimishaji, mihadhara na maonesho kama Sabasaba, wananchi hupatiwa maarifa kuhusu madhara ya kutumia dawa bila ushauri wa wataalamu wa afya.
Elimu hii inalenga kubadilisha mtazamo wa jamii na kuhimiza tabia ya kutafuta huduma za afya kutoka kwa wataalamu badala ya kujitibu.

Katika juhudi za kuimarisha uelewa huo, TMDA pia huhamasisha wananchi kuripoti dawa duni, bandia au zenye madhara kupitia mifumo ya kielektroniki.
Ushirikishwaji huu wa jamii unasaidia mamlaka kupata taarifa kwa haraka na kuchukua hatua stahiki, ikiwa ni pamoja na kuondoa bidhaa hatarishi sokoni na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo, anasisitiza kuwa mamlaka hiyo itaendelea kuimarisha ukaguzi wa dawa katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha usalama wa wananchi.

“Sisi jukumu letu ni kuhakikisha kwamba dawa inatumika kama ilivyokusudiwa na siyo kumdhuru mtumiaji. Tunahakikisha tunasajili dawa zote zinazokidhi vigezo ili kulinda afya ya Mtanzania,” anasema.
Anaongeza kuwa, TMDA hufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maduka ya dawa, masoko na mipakani ili kudhibiti uingizaji na usambazaji wa dawa zisizo salama.
“Tunafanya ukaguzi kila siku katika maeneo mbalimbali ikiwemo mipakani na kwenye maduka ya dawa ili kuhakikisha kuwa bidhaa zote zinazoingia na kuuzwa nchini zinakidhi viwango vya ubora na usalama,” amesema Dkt. Fimbo.
Aidha, anaeleza kuwa mamlaka ina maabara za kisasa zenye viwango vya kimataifa zinazotumika kupima ubora wa dawa na kuhakikisha zinakuwa salama kwa matumizi ya binadamu.

“Tunapima dawa zetu katika maabara zenye ubora wa kimataifa unaotambuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), jambo linalotupa uhakika wa ubora wa dawa zinazotumika nchini,” anasema.
Katika hatua nyingine, Dkt. Fimbo anatoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kutumia dawa kiholela bila kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.
Anasisitiza kuwa matumizi mabaya ya dawa yanachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa usugu wa dawa, hali ambayo ni hatari kwa afya ya jamii kwa ujumla.
“Ni muhimu kwa wananchi kuelewa kuwa si kila ugonjwa unahitaji kutumia dawa bila uchunguzi. Wanapaswa kufuata maelekezo ya wataalamu ili kuepuka madhara yasiyo ya lazima,” ameonya.
Kwa ujumla, juhudi za TMDA katika kupambana na matumizi ya dawa kiholela zina mchango mkubwa katika kulinda afya ya jamii.
Kupitia usajili wa dawa, ukaguzi wa mara kwa mara, udhibiti wa matangazo, ufuatiliaji wa ubora wa dawa sokoni na utoaji wa elimu kwa umma, mamlaka imeendelea kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata dawa salama na zenye ufanisi.
Hata hivyo, mafanikio ya juhudi hizi yanategemea pia ushirikiano wa wananchi. Kila mmoja anapaswa kuchukua jukumu la kufuata ushauri wa wataalamu wa afya, kuepuka kujitibu, na kuripoti changamoto zozote zinazohusiana na dawa.
Kupitia ushirikiano huu kati ya TMDA na jamii, inawezekana kupunguza kwa kiasi kikubwa au hata kumaliza kabisa tatizo la matumizi ya dawa kiholela nchini, na hivyo kujenga taifa lenye afya bora na salama kwa wote.


