Na Tatu Mohamed
ZAIDI ya wafanyakazi wa majumbani 700 wamepatiwa mafunzo maalum na kutunukiwa vyeti na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kwa lengo la kuwawezesha kupata ujuzi mahususi kwa kazi zao.
Kwa mujibu wa Muwezeshaji wa mradi huo, Debora Mwageni, mafunzo hayo yanamwezesha mfanyakazi wa ndani kuwa na uwezo wa kushiriki majadiliano yenye lengo la kuboresha mazingira ya kazi pamoja na kupata maslahi bora.
Akizungumza katika banda lao kwenye Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) 2025, Debora amesema mradi huo ulianza Aprili mwaka jana na umepokelewa kwa muitikio mkubwa.

“Wafanyakazi wa ndani wanasaidiwa kuelewa majukumu yao, haki na wajibu wao katika kazi wanazofanya,” amesema.
Aidha, amesema kupitia mradi huo, wafanyakazi hao wanawezeshwa kupata ajira za kudumu, kulinda afya zao na kuhakikisha mazingira ya kazi yanakuwa salama.
Mafunzo hayo yanahusisha masuala mbalimbali kama vile uandaaji wa chakula, usimamizi wa nyumba, usafi, kufua na kunyoosha nguo, pamoja na malezi ya watoto na wazee.
Debora ameongeza kuwa mafunzo pia yanawaandaa kwa ajili ya kufanya kazi katika nchi za nje kama vile Dubai, Oman, Denmark, Uingereza, Marekani na Italia.

“Tunawapa ujuzi wa stadi za maisha, elimu ya afya ya uzazi, pamoja na mbinu bora za kuwahudumia watu wanaoishi nao kwa ukarimu huku wakifahamu haki zao za msingi,” amesema.
Ameeleza kuwa wafanyakazi wa ndani ni sawa na wafanyakazi wengine, hivyo wanapaswa kupata heshima stahiki na kutambuliwa rasmi.
Debora amewashauri Watanzania kujiwekea utamaduni wa kupata elimu na mafunzo kabla ya kuajiriwa ili kujiimarisha katika kazi zao.