Na Tatu Mohamed
KATIKA hatua ya kuleta mageuzi katika usimamizi wa matumizi ya maji nchini, Chuo cha VETA Pwani kupitia kwa Mwalimu wao, Khamis Salum, kimebuni mfumo wa kisasa wa Mita ya maji unaotuma taarifa moja kwa moja kwenye mfumo wa kidijitali.
Akizungumza katika banda lao lililopo katika Viwanja vya Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam ‘Sabasaba’ Mwalimu Khamis amesema kuwa Mita hiyo ni tofauti na zile zilizozoeleka majumbani ambazo huhitaji kusomewa moja kwa moja katika eneo ilipo.
Amesema mfumo huo mpya unafanya kazi kwa njia ya kielektroniki na kuondoa changamoto ya usomaji wa mita kwa mikono.

“Kwa kawaida, mtu alipaswa kwenda hadi kwenye mita ili aisome. Lakini mfumo huu wa sasa unatuma taarifa moja kwa moja kwenye mfumo wa kielektroniki. Hii husaidia kupata taarifa kwa wakati na kuondoa usumbufu wa wateja kushare mita moja,” amesema Khamis.
Kwa mujibu wa maelezo yake, mfumo huo unatatua matatizo makubwa mawili: kwanza ni ucheleweshwaji wa taarifa za matumizi ya maji, na pili ni changamoto ya wapangaji wengi kutumia mita moja na hivyo kusababisha migogoro ya bili.
“Hii mita mpya inaruhusu matumizi ya kadi binafsi zilizosasishwa kwa majina ya watumiaji. Mteja anapoweka kadi yake, mfumo unamtambua na kutoa maji kulingana na salio alilonalo. Maji hukoma mara tu salio linapoisha au kadi inapotolewa,” amefafanua.

“Mbali na kusaidia kutatua migogoro baina ya wapangaji, mfumo huu pia utapunguza matatizo ya bili za kubambikiwa ambazo zimekuwa kero kwa wananchi wengi,” ameongeza Mwalimu Khamis.
VETA imekuwa ikihamasisha ubunifu miongoni mwa wanafunzi wake kwa lengo la kutatua changamoto za kijamii kwa kutumia teknolojia na maarifa ya fani wanazosomea.
Ubunifu huo uliobuniwa ndani ya kipindi cha miezi mitatu katika Chuo cha VETA Pwani, unalenga kuleta mapinduzi kwenye usimamizi wa huduma za maji, hasa katika maeneo yenye nyumba za kupanga ambazo hukumbwa na migogoro ya mara kwa mara kuhusu matumizi ya maji.
Mfumo huu wa Mita ya maji ni ushahidi kuwa elimu ya ufundi stadi inaweza kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.