Na Mwandishi Wetu
Mkuu mpya wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi amesema atafanya kazi aliyotumwa na Rais Samia Suluhu Hassani na hataruhusu kikwazo chochote kitakachojaribu kuzuia maendeleo ya wananchi.
Akizungumza wakati wa kukabidhiwa ofisi leo Juni 30,2025 na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, Kihongosi amesema ataendeleza pale pale alipoishia mtangulizi wake ili kusonga mbele lengo kila mwananchi wa Arusha aweze kufurahia matunda.

“Mheshimiwa Rais aliponiteua naamini wote mlisikia, kuna kazi alinituma na alizungumza hadharani. Ajenda yetu kubwa ni wananchi kuwa na imani na Serikali yao, fedha zinaletwa, miradi inajengwa kazi yetu ni kwenda kuisimamia,” ameeleza.
Aidha Kihingosi amewaomba watumishi wenzake wa umma kushirikiana katika kazi waliyoaminiwa ili kuhakikisha wananchi wanapa kile walichokitarajia.
“Mhe Rais amenituma Arusha kuja kuwatumikia wananchi wa Arusha na nimekuja kufanya kazi, ninachoomba kwenu ni ushirikiano ili kusukuma mbele gurudumu la Maendeleo, tukiwa na lengo la kuhakikisha wananchi wa Arusha wanafurahia matunda ya nchi yao,” amesema Kihongosi.

Kwa upande wake, Makonda wakati akitoa hotuba yake ya kuwaaga wakazi wa Arusha, ameweka wazi kuwa anavyofahamu uchapakazi wa Kihongosi na hana mashaka naye na kumtaka kuendelea kuwatumikia wananchi wa Arusha, huku akimsisitiza umuhimu wa ushirikiano na mshikamano kati yake na viongozi wa mkoa huo wakiwememo viongozi wa Chama na Serikali, viongozi wa dini, wadau na wananchi wa ngazi zote.
“Nina imani kuwa Mkuu mpya wa Mkoa, Mheshimiwa Kenan Kihongosi, ataendeleza jitihada zote tulizoanza na kuongeza ubunifu mpya katika kuleta maendeleo ya wananchi wa Arusha, nikuhakikishie wananchi wa Arusha wote ni wajanja na wapenda maendeleo” amesema Makonda.

Kihongosi amehamishiwa mkoani Arusha akitokea Mkoa wa Simiyu ambapo wakati wa kuapishwa Rais Samia alimtaka kutumia nguvu aliyotumia Simiyu, akatumie Arusha agizo mojawapo ikiwa ni kuwaunganisha wananchi wa mkoa huo.