Kweli IJP Wambura Polisi wamefanikiwa, sasa umma unataka kujua wasiojulikana

JUMATATU wiki hii Jeshi la Polisi lilikuwa na mahafali ya maofisa wa vyeo vya inspekta wasaidizi wa polisi ambayo yalifanyika katika chuo cha maofisa wa Polisi Kurasini jijini Dar es Salaam. Waliohitimu ni wale walioanza mafunzo ya kwanza kwa mwaka 2024/25. Mafunzo hayo yalifungwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu.

Kama ilivyo ada, ziliwasilishwa hotuba kadhaa, ikiwamo ya Rais Samia mwenyewe ambaye alionyesha kufurahishwa na kuridhika na kazi inayofanywa na Jeshi la Polisi katika wajibu wake mkuu wa kulinda raia na mali zao. Wengine waliotoa hotuba ni pamoja na Mkuu wa Chuo hicho Lazaro Mambosasa ambaye alieleza kwa kina mafunzo yaliyotolewa mahali hapo, kabla ya Rais kutoa hotuba yake Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenarali wa Polisi, Camillus Wambura, ambaye alizungumza kwa kina jinsi polisi wamefanikiwa katika kukomesha uhalifu nchini.

Kwa mfano, IJP Wambura alisema kwamba kati ya uhalifu ambao polisi wamekomesha ni pamoja na vitendo vya utekaji wa magari katika barabara kuu. Vitendo hivi alisema vilikuwa ni vingi nchini katika barabara kuu, lakini sasa vimekuwa ni historia. Alitaja pia migogoro na mapigano baina ya wakulima na wafugaji kwamba wameyakomesha; mafanikio mengine ambayo IJP alitaja ni pamoja na kukomesha ‘Panya Road’ waliokuwa wanatikisa katika miji mikubwa nchini kama Dar es Salaam; kukomesha ujambazi wa kuvunja nyumba na kupora katika miji mikubwa nchini; kukomesha uvamizi wa vituo vya mafuta matukio ambayo yalikuwa yamekithiri nchini. Mafanikio mengine ni kukomesha uporaji wa fedha kwa kutumia bodaboda; kwa ujumla IJP Wambura alisema kwamba wamekomesha vikundi vya uhalifu vilivyokuwa vimeota mizizi nchini kama kikundi cha ‘10 Ndani 10 Nje’ kilichokuwa kinasumbua jijini Dar es Salaam; ‘Kanyaga Twende’ kilichotikisa Arusha, kutaja kwa uchache tu.

IJP Wambura alifungamanisha mafanikio hayo na mambo kadhaa, kubwa ni kuongezeka kwa morali ya kazi kwa askari polisi kwa kuwa maslahi yao yameboreshwa; wamepandishwa ngazi kwa wakati; wamepatiwa vitendea kazi vya kisasa zaidi na kujengewa nyumba mpya kwa ajili ya ofisi na makazi.

Katika mahafali hayo IJP Wambura alisema kwamba Chuo Cha Polisi (CCP) Moshi kimejengwa upya kwa kuondoa majengo ya zamani ya kikoloni. Hatua za ujenzi zimefikia pazuri, na kwamba ujenzi huo ukikamilika CCP itakuwa na sura mpya kabisa.

IJP Wambura alisema kwamba wamejipanga vema kuhakikisha kwamba Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 unafanyika kwa amani na utulivu. Aidha, alisema: “Tuna wivu mkubwa na amani ya nchi yetu.” Kauli hiyo ilikuwa ni kuthibitisha kwamba Jeshi la Polisi halitaruhusu wala kuvumilia vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu ili nchi iendelee kubaki kuwa ya amani na salama.

Kwa hakika kauli za IJP Wambura juu ya mafanikio ya Jeshi la Polisi kwa kipindi cha uongozi wake, ni makubwa kama yeye mwenyewe alivyoyafafanua. Ni kweli vitendo vya uhalifu uliokuwa unafanywa na vikundi vya kihalifu vimepungua, ni kweli pia matukio ya kutekwa magari na zama za mabasi kuzuiwa kutembea baadhi ya maeneo ya nchi nyakati za usiku kwa hofu ya majambazi waliokuwa wanateka magari, hasa ukanda wa magharibi mwa nchi, yamekuwa historia. Panya Road nao ni kama wametoweka, ingawa bado vibaka wanasumbua kwenye makazi ya watu. Ni kweli IJP Wambura ana haki ya kujivunia mafanikio haya.

Mafanikio haya pia yametajwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa, akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa wizara hiyo kwa mwaka 2025/26. Aliliambia Bunge kuwa jumla ya magari 218 yalipokewa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya matumizi ya Makamishna, Naibu Kamishna, Makamanda wa Polisi wa Mikoa/Vikosi, Wakuu wa Polisi Wilaya na Vitengo ndani ya Jeshi la Polisi, pamoja na pikipiki 105 za Polisi Kata na Shehia.

Ingawa magari na pikipiki siyo kila kitu katika utendaji wa Jeshi la Polisi, hata hivyo, Waziri alisema kuwa upatikanaji wake umeimarisha utolewaji wa huduma kwa wananchi.

Tunapotafakari taarifa za viongozi wa polisi na hata za Waziri kuhusu mafanikio ya Jeshi la Polisi, zinaibuka hisia mchanganyiko. Hizi ni kwamba kwa nini katika mawanda ya mafanikio ya kiwango hiki katika kukomesha uhalifu na upatikanaji wa vitendea kazi, bado nchi imejaa hofu na woga wa watu kupotea au kupotezwa na watu wasiojulikana? Ni kwa nini katika matukio yote makubwa ambayo yameripotiwa ya kupotea kwa watu, polisi hawajui kilichotokea?

Hili swali linasumbua vichwa vya wananchi wengi, kwamba katika uwezo, nguvu na mtandao wa Jeshi la Polisi, inakuwaje haina taarifa za kina za watu wanaopoteza au kupotezwa, au haina taarifa za hawa wanaofanya matendo haya maovu ambayo yanachafua sura na sifa njema ya taifa letu?

Kama polisi wamekomesha haya yote ambayo IJP Wambura amesema, inakuwaje inakuwa vigumu kukomesha matendo haya ya kupotezwa, kutekwa na hata kuuawa kwa watu katika mazingira ya kutatanisha?

Tangu mwaka jana ilipowekwa hadharani orodha ya watu zaidi ya 80 wanaoaminika ama wamepotea, au wametekwa au wameuawa au hawajulikani waliko, huku kidole cha tuhuma kikielekezwa kwa Jeshi la Polisi, hadi leo hakuna taarifa yoyote ya uchunguzi kuhusu hatma ya raia hao. Hata pale Amiri Jeshi Mkuu alipotaka ufanyike uchunguzi wa kuuawa kwa aliyekuwa Kada wa Chadema Ali Kibao, hakuna taarifa ambayo imewekwa wazi. Mazingira ya kukamatwa na kisha kuuawa kwa Kibao, yaliacha maswali na mashaka makubwa kwa umma, huku tuhuma zikielekezwa kwa Jeshi la Polisi.

Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba IJP Wambura anaweka wazi mafanikio ya Jeshi la Polisi katika miaka ya hivi karibuni, lakini wakati huo huo Jeshi hilo likishindwa kuwapa wananchi majibu ya maswali ya utekaji. Umma unahoji kila uchao ni nani hasa wanaoteka wananchi? Jeshi la Polisi limekana na kujiweka kando kuhusika na kadhia zote hizi. Polisi wamesema na kusisitiza kuwa hawahusiki na utekaji na mauaji yanayoripotiwa kuhusiana na uhalifu wa watu wasiojulikana.

Wakati tukipokea mafanikio ya Jeshi la Polisi kama yalivyofafanuliwa na IJP Wambura na kwa kweli kuungwa mkono na wote walioshiriki hafla ya mahafali ya maofisa wa polisi Jumatatu wiki hii katika Chuo cha Maofisa wa Polisi Kurasini, ni vema ikajulikana kwamba umma bado unasubiri kupata majibu kutoka kwa polisi juu ya ni nani hasa anateka. Nani anapoteza na kuua raia chini ya kivuli cha watu wasiojulikana? Umma unahoji haya kwa sababu unajua kuwa Jeshi la Polisi lina uwezo, nyenzo na maarifa ya kuwajua watesi wa raia ni akina nani.

spot_img

Latest articles

Kamishna wa umeme na Nishati Jadidifu afanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya umeme Dar

▪️Aridhishwa na hatua ya utekelezaji wa miradi
 ▪️Awataka wakandarasi kuzingatia viwango na TANESCO kuongeza usimamizi...

Kampeni ya pika Smart inayohamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia yazinduliwa

📌 Kamishna Luoga asisitiza matumizi ya umeme katika Nishati Safi ya Kupikia Na Mwandishi Wetu...

Wizara ya Elimu yazindua kituo cha huduma kwa wateja

Na Mwandishi Wetu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imezindua Kituo cha Huduma kwa wateja,...

Watanzania  wako tayari kuchangia  harusi, sio gharama za matibabu ya mtoto- Dk. Mollel

Na Mwandishi Wetu Serikali imetoa wito kwa wananchi kubadilika na kuwekeza katika bima ya afya...

More like this

Kamishna wa umeme na Nishati Jadidifu afanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya umeme Dar

▪️Aridhishwa na hatua ya utekelezaji wa miradi
 ▪️Awataka wakandarasi kuzingatia viwango na TANESCO kuongeza usimamizi...

Kampeni ya pika Smart inayohamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia yazinduliwa

📌 Kamishna Luoga asisitiza matumizi ya umeme katika Nishati Safi ya Kupikia Na Mwandishi Wetu...

Wizara ya Elimu yazindua kituo cha huduma kwa wateja

Na Mwandishi Wetu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imezindua Kituo cha Huduma kwa wateja,...