WIKI iliyopita Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiliweka hadharani ilani yake ya uchaguzi kwa kipindi cha mwaka 2025 – 2030. Ni ilani ambayo imesheheni mambo mengi ambayo kama chama hicho kitapata ridhaa ya wananchi katika uchaguzi mkuu mwaka huu, basi ndiyo ambayo yatatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Miongoni mwa mambo ambayo ilani hiyo imegusia ni masuala ya kudumisha demokrasia
na utawala bora. CCM inasema kwamba katika kipindi cha utekelezaji wa Ilani hiyo,
itaielekeza Serikali kuendelea kuimarisha demokrasia na utawala wa sheria kwa kuimarisha misingi ya demokrasia. Haya ni kama vile kuboresha mazingira wezeshi ya wananchi kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa kuzingatia maadili na sheria za nchi; pia itahuisha na kukamilisha mchakato wa katiba mpya.
Katika mlolongo mambo ya demokrasia na utawala bora CCM inaeleza kuwa itafanyia kazi
Mapendekezo ya Tume ya Rais ya Haki Jinai, kwa kuhuisha mfumo wa nyumba kumi kisheria.
Itakumbukwa kwamba tarehe 31 Januari, 2023, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Samia Suluhu Hassan, alizindua Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai nchini chini ya Mwenyekiti Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Chande Othman, Makamu Mwenyekiti Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Balozi Ombeni Yohana Sefue na wajumbe tisa pamoja na Sekretarieti yake. Nia ya kuundwa kwa Tume hiyo ilikuwa ni kumsaidia Rais kupata ushauri na mapendekezo juu ya namna bora ya k uboresha mfumo na utendaji kazi wa taasisi zinazohusika na Haki Jinai.
Tume hiyo ilipendekeza kuimarishwa kwa mfumo wa matumizi ya kamera za ulinzi (CCTV) na TEHAMAkatika kubaini na kuzuia uhalifu na wahalifu; Kuanzisha mamlaka mpya na huru ya upelelezi inayojitegemea itakayojulikana kama Ofisi ya Taifa ya Upelelezi (National Bureau of Investigation) itakayokuwa na jukumu la kupeleleza makosa yote ya jinai; na kuboresha mishahara na maslahi ya askari wa Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, na Uhamiaji ikiwamo
kupitia upya umri wa kustaafu na mafao ya pensheni.
Aidha, Tume ilibaini kwamba taifa limegubikwa na tabia ya matumizi mabaya ya madaraka ikiangazia vyombo vyenye mamlaka ya kukamata watuhumiwa wa uhalifu na kuzuia uhalifu kuwa kwa nyakati mbalimbali vimekuwa vikitumia vibaya mamlaka yake ya ukamataji, hivyo kusababisha bughudha na kero kwa wananchi. Mathalan, kukamata watu bila sababu na kukamata watu kwa makosa ya madai.
Ni katika muktadha huo, Tume pamoja na mambo mengine ilipendekeza kwamba Jeshi la Polisi lifanyiwe tathmini ya kina itakayowezesha kufanyiwa maboresho makubwa na kuundwa upya ili kuondoa kasoro za kiutendaji zilizopo; Jeshi la Polisi libadilishwe kisheria, kimuundo na kifikra na kuwa Polisi Tanzania (National Police Service). Mabadiliko hayoyatatoa taswira kuwa Jeshi la Polisi ni chombo cha kuwahudumia wananchi; pia ilipendekeza kubadilisha mitaala ya mafunzo na mtazamo wa askari wa Jeshi la Polisi ili kutoka katika dhana ya ujeshi (police force) kwenda dhana ya kuhudumia wananchi (police service).
Uamuzi wa CCM kutumia ripoti ya Tume ya Haki Jinai katika kuandaa ilani yake, inaonyesha utayari wa kufanyia kazi mapendekezo yake ili kusaidia kujenga mazingira ya utawala bora na demokrasia nchini. Ni jambo la kupongeza.
Hata hivyo, nyakati tunazoishi sasa zimethibitisha pasi na shaka yoyote kwamba kile ambacho Tume ya Haki Jinai ilisema, siyo tu kimezidi kudhihirika, bali pia kimekithiri sana. Katika siku za hivi karibuni umma umeshuhudia matumizi mabaya kabisa ya mamlaka ya kipolisi. Hii ni kuanzia kukamata watuhumiwa, kuwashikilia katika vituo vya polisi na hata wakati wa kusindikiza watuhumiwa mahakamani kuna ukatili mwingi unatendeka. Kuna ukiukaji wa haki za watuhumiwa, na hata za raia ambao hawana kabisa tuhuma yoyote. Hali inazidi kuwa mbaya kila uchao.
Ilitarajiwa kwamba ripoti ya Haki Jinai ingelikuwa nyenzo muhimu ya kusaidia kusukuma mabadiliko mengi ya kimfumo katika maeneo mengi ambayo yametajwa katika nyanja za haki jinai. Kwa bahati mbaya, mengi bado hayajafanyiwa kazi, na haielekei kama yatafanyiwa kazi katika siku za hivi karibuni.
Pengine ni jambo la bahati mbaya kwamba taifa letu limekuwa na utamaduni wa kuepuka kukubali mabadiliko hata pale yanapokuwa yamependekezwa na tume ambazo zimeundwa na serikali yenyewe. Hili liko dhahiri. Kumbukumbu za ama kupuuzwa au kubezwa kwa ripoti za tume zilizoundwa na serikali zingali hai miongoni mwa Watanzania. Kwa mfano, Tume ya Jaji Robert Kisanga ya mabadiliko ya katiba ilikutana na rungu zito la Rais Benjamin Mkapa; Tume ya Jaji Francis Nyalali kuhusu mfumo wa kisiasa nchini nayo haikupona rungu hili, licha ya kukubaliwa kwa mfumo wa vyama vingi kutoka chama kimoja mapendekezo mengi ya mabadilko ya sheria kandamizi hayakupokewa vizuri na watawala. Vivyo hivyo, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba nayo haikutoka salama.
Pamoja na kutambua nafasi ya ripoti ya Haki Jinai katika ilani ya CCM ya mwaka 2025 -2030, na tukipongeza hatua hiyo, bado ni dosari kubwa kwa kuchukua vitu vichache kiasi hiki. Utajiri wa mapendekezo yaliyoko katika ripoti hiyo hayajachukuliwa kwa uzito unaostahili, hasa katika eneo la kuona kwamba Jeshi la Polisi linakwenda kufanyiwa mabadiliko makubwa ili liwe chombo rafiki kwa raia na siyo chombo chenye sura ya jeshi la kikoloni la kuumiza raia tena kwa kuwaonea.
Inawezekana kwamba kwa kuwa ilani inasema inakwenda kuhuisha mchakato wa katiba mpya ambao umekwama kwa zaidi ya miaka 11 sasa, huenda na masuala mengine mengi ambayo Tume ya Haki Jinai iliyataja, yatapata ufumbuzi kama kweli Tanzania itapata katiba mpya. Ni jambo jema kuwa na matumaini chanya kwamba hayo yatakwenda kutokea.
Hata hivyo, ni vema kuwa na tahadhari mapema, miaka 11 iliyopita kama siyo kupotea katika kupata Katiba mpya imekuwa ni hasara kwa Watanzania wote. Yawezekana kuna wanaodhani au kuamini kwamba mambo yalivyo sasa yanawapa unafuu na faida zaidi kuliko kuwa na katiba mpya. Inawezekana wenye mawazo hayo wakawa wanavutia kwao, lakini ni vizuri zaidi wakumbuke kwamba uongozi ni kupeana vijiti, ni kuwa zamu kwa kipindi chako na kuondoka. Ni hakika muda mwingi watu wanaishi wakiwa nje ya nafasi za madaraka waliyokalia kwa kitambo kidogo tu. Hii ni dhahiri, iwe kwenye ofisi ya umma ulioajiriwa, iwe kwenye ofisi ya kampuni binafsi au hata kwenye ofisi ya kisiasa ya kuchaguliwa.
Hali hii inatoa ilani kwamba ni vema kujenga mazingira ya kuhakikisha kuwa mifumo yetu na utendaji wake vinaleta utulivu wakati wote, iwe upo umekalia kiti au uko nje. Mapendekezo yanayotolewa mara nyingi na hizi tume ambazo hata hivyo huundwa na serikali yenyewe tena kwa kuchagua watu inayowaamini, yanalenga kujenga Tanzania bora na njema zaidi kesho kuliko ilivyo leo. Tukubali kubadilika.