Kiburi cha madaraka, mfereji wa matusi havitajenga EAC

JUMUIYA ya Afrika Mashariki iliyovunjika mwaka 1977 yalikuwa ni matokeo ya kuwa kwenye msukosuko kwa miaka sita. Hali hii ya msukosuko ilichangiwa sana na kuangushwa kwa utawala wa Milton Obote, Rais wa Uganda mwaka 1971. Mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Iddi Amin nchini Uganda yalimfanya Obote akimbilie Tanzania ambako alipewa hifadhi ya kisiasa na utawala wa Mwalimu Julius Nyerere.

Kutokana na misukosuko hiyo, kuhisiana vibaya, kushutumiana na hatimaye kuiva kwa mgogoro huo kiasi cha wakuu wa nchi za Jumuiya hiyo, Mwalimu Nyerere (Tanzania) Mzee Jomo Kenyatta (Kenya) na Iddi Amin kushindwa kukutana kwenye vikao rasmi. Kwa ujumla hali hii ilichochea sana kuzorotesha ari na ushirikiano wa Jumuiya hiyo. Hali hii ilizidi kujenga nyufa katika Jumuiya kiasi cha kuifanya isiweze kusimama tena na matokeo yake Julai 1977 ilivunjika na kuacha hasara kubwa ya kiuchumi, kijamii na kisiasa baina ya nchi zote wanachama.

Juhudi za kufufuliwa kwa Jumuiya hii zilikuja kuzaa matunda miaka 23 baadaye. Katika juhudi za kufufuliwa kwa Jumuiya hii ilitarajiwa katika mkataba wake uliosainiwa Novemba 1999 na kisha kuanza kutumika Julai 2000, iwe ni ya kuwaleta pamoja Wanaafrika Mashariki ili kujenga uchumi bora wa nchi wanachama. Kwamba jumuiko hili lisaidie nchi hizi kupambana dhidi ya umasikini kwa kuunganisha nguvu katika kushirikiana kwenye nyanja za ushuru wa forodha, soko la pamoja, sarafu moja na mwishowe shirikisho la kisiasa baina ya nchi wanachama.

Sasa ni takribani miaka 25 tangu Jumuiya ya pili ianze mwaka 2000, zipo hatua nyingi zimepigwa kwenye nyanja za ushuru wa forodha na soko la pamoja, lakini bado kuna kazi ngumu ya kufikiwa kwenye nyanja za sarafu moja na shirikisho la kisiasa.

Hata hivyo, pamoja na juhudi za mafanikio haya na changamoto zilizoko, nchi wanachama zimeendelea na ‘jadi’ yao ya kuhisiana vibaya, kutendeana mabaya na kuna kila dalili kwamba bado kuna chuki inapikwa ama na baadhi ya makundi ya watu katika Jumuiya na hata pengine kuchochewa na baadhi viongozi japo kwa uficho.

Hivi karibuni lilitokea tukio lisilopendeza la baadhi ya raia wa Kenya na Uganda kuzuiwa kuingia nchini baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Walirejeshwa walikotoka, na wengine ambao walikuwa tayari wamekwisha kuingia mjini, walisakwa na kushikiliwa na vyombo vya usalama vya Tanzania kisha kurejeshwa kwao, Kenya na Uganda.

Katika kadhia hii ambayo inahusika na kesi zilizoko mahakamani za uhaini na uchochezi dhidi ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, imeamsha fadhaa kubwa. Waliozuiwa kuingia nchini walikuwa wanafuatilia kesi hizo. Kumekuwa na malalamiko jinsi walivyotendwa, baadhi wakidaiwa kusafirishwa kwa njia ambazo haziko wazi kisha kutupwa mpakani mwa Kenya na Tanzania na pia kati ya mpaka wa Uganda na Tanzania. Kote huko wanakodaiwa kutupwa, taratibu mahususi za kiuhamiaji hazikufuatwa. Mosi, kwa sababu hakukuwa na kukabidhiana kwa wahusika kwa mamlaka za nchi jirani, lakini pia njia zilizotumika kuwasafirisha zinaelezwa kuwa ni za kiudhalilishaji.

Pia kumekuwa na madai kwamba baadhi ya raia hawa, mmoja wa Kenya na mwingine wa Uganda, walipigwa, wakaumizwa, wakadhalilishwa, huku wakishikiliwa bila kupata fursa ya kuwasiliana ama na ndugu zao au mawakili wao, kabla ya kurejeshwa makwao kwa njia zilizojaa utata mwingi.

Tukio hili limeamsha taharuki kubwa baina ya wananchi wa Tanzania na Kenya. Kumekuwako na mijadala mikali yenye jazba kubwa kwenye mitandao ya kijamii juu ya kadhia hii. Kikubwa ambacho kimeteka mitandao ya kijamii ni lugha za matusi ambazo zinamlemga kiongozi mkuu wa Tanzania, lakini na Watanzania wote kwa ujumla wake.

Baadhi ya kauli hizi za kutusi na kudhalilisha hazivumiliki. Hazivumiliki kwa sababu moja kubwa, kwanza siyo Watanzania wote kwa ujumla wao walihusika na kadhia ya kuzuia raia hao wa Kenya na Uganda kuingia nchini. Pia siyo Watanzania wote walioshiriki kuwatesa kama inavyodaiwa au hata kuwasafirisha katika njia ya kuwatweza kama inavyodaiwa. Kwa maana hiyo kuwatusi Watanzania wote ni kuwabebesha lawama ambazo hawastahili.

Hata hivyo, kufurumusha matusi kwa kiongozi mkuu wa nchi, bado siyo utatuzi wa jambo hili, kwa sababu hakuna hata siku moja matusi yalipata kutatua tatizo. Matusi badala ya kutatua matatizo huyaongeza na kuzidi kujenga uadui pale ambako liko jambo linalostahili kutafutiwa ufumbuzi.

Kwa hali ya mambo yanayoendelea kwenye mitandao ya kijamii, picha moja muhimu sana inajitokeza juu ya uhusiano wa raia wa nchi hizi, hasa Tanzania na Kenya. Inajitokeza sura ambayo inaonyesha kwamba miaka hii 25 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki haijaweza kuwaweka karibu raia wa nchi hizi mbili, hivyo kujenga ukaribu, kuheshimiana na kuwa na staha kila mmoja anapozungumza kuhusu mwingine. Kuna uhusiano wa mashaka, tena mashaka makubwa.

Pili mamlaka zetu katika nchi hizi, bado zinakabiliwa na tatizo la kukosa weledi katika kushughulikia mambo nyeti kuhusu raia wa nchi wanachama. Kuna kila dalili kwamba chuki inatangulia hekima, sheria na taratibu katika kushughulikia masuala yanayohusu raia wa upande wa pili wa mpaka.

Ni rahisi sana kuona kwamba mambo haya ni madogo, lakini ukweli ni kwamba kama tuna kumbukumbu nzuri, yaliyotokea mwaka 1977 kwa kuvunjika kwa ile Jumuiya ya awali iliyoanza mwaka 1967, ni matokeo ya kupuuza mambo. Upuuzaji wa viongozi wa nchi wanachama kutatua kutokuelewana baina yao, kushindwa kuheshimu kila nchi mwanachama kwa kadri alivyo, lakini kikubwa zaidi ile tu kushindwa kuona thamani kubwa ya Jumuiya miongoni mwa wananchi wa nchi hizi.

Haya ya safari hii ya kuwatenda raia wa Kenya kama ambavyo wanadaiwa kutendewa, hakika imezidi kujenga chuki baina ya wananchi wa nchi hizi mbili.

Inasikitisha kuona sasa vita ya matusi imetamalaki kwenye mitandao ya kijamii, wapo watu wamejipa kazi ya kutunga vikaragosi vya kumdhalilisha kiongozi mkuu wa nchi ya Tanzania; wapo ambao wamepata mwanya wa kuwafurumushia matusi Watanzania wote, na kwa kweli kwa maoni yangu juhudi zote hizi hazina nia njema katika kuifanya Jumuiya ya Afrika Mashariki ipige hatua kubwa zaidi ya maendeleo katika ushirikiano baina ya nchi wanachama.

Pengine tukio hili la kusikitisha ambalo sasa limekuwa ndiyo kichocheo cha kufunguliwa kwa milango ya matusi, kebehi na kila aina ya udhalilishaji baina ya watu wa mataifa haya, litakuwa ni fundisho kwa wenye mamlaka katika nchi hizi kujiuliza mara mbili mbili kabla ya kuchukua maamuzi ambayo yatakwenda kubomoa Jumuiya badala ya kuijenga. Tusidanganyane, tunahitajiana wote ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, siyo kiburi cha watendaji wa vyombo vya dola, wala mfereji wa matusi vitajenga Jumuiya hii. Kila mmoja ajifunze kuwa na kiasi.

spot_img

Latest articles

Bodi ya wakurugenzi Ewura yatembelea miundombinu ya Gesi Asilia iliyoshindiliwa (CNG)

Na Mwandishi Wetu BODI ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati...

Wadau watoa tahadhari kuhusu Haki za Kidijitali kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025

Na Mwandishi Wetu MASHIRIKA mawili makubwa yanayojihusisha na haki za kidijitali ya Paradigm Initiative...

REA yahamasisha wananchi kutumia Mkaa Mbadala

📌Yasisitiza ni salama, gharama nafuu na ni rafiki wa mazingira 📌Yathibitisha kuendelea kuwawezesha wazalishaji wake WAKALA...

Serikali yasisitiza Dabi iko pale pale Juni 15

Na Mwandishi Wetu Wakati Yanga ikiendelea na kampeni yake ya ‘Hatuchezi’ Serikali imethibitisha rasmi kuwa...

More like this

Bodi ya wakurugenzi Ewura yatembelea miundombinu ya Gesi Asilia iliyoshindiliwa (CNG)

Na Mwandishi Wetu BODI ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati...

Wadau watoa tahadhari kuhusu Haki za Kidijitali kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025

Na Mwandishi Wetu MASHIRIKA mawili makubwa yanayojihusisha na haki za kidijitali ya Paradigm Initiative...

REA yahamasisha wananchi kutumia Mkaa Mbadala

📌Yasisitiza ni salama, gharama nafuu na ni rafiki wa mazingira 📌Yathibitisha kuendelea kuwawezesha wazalishaji wake WAKALA...