Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeendelea kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuzalisha fursa za ajira nchini kupitia uwekezaji na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki, reli ya kisasa, Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato.

Amesema katika kipindi cha Novemba 2020 hadi Februari, 2025 jumla ya ajira 8,084,204 zimezalishwa katika sekta ya umma na sekta binafsi.
Majaliwa amesema hayo leo Aprili 09,2025 wakati akitoa hotuba yake kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2025/2026.

“Vilevile, Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kukua na kupanua wigo wa uzalishaji wa ajira nchini, kutokana na jitihada hizo, katika kipindi cha Novembea 2020 hadi Februari, 2025 jumla ya ajira 8,084,204 zimezalishwa katika sekta ya umma na sekta binafsi,” amesema.