Makalla aisaidie Polisi, Wizara ya Afya kuhami Watanzania

TANZANIA ilipata kushuhudia wanasiasa wasiotabirika, wenye kauli za kuchanganya na hadaa nyingi. Wapo ambao kusema uongo mchana kweupe kwao siyo tatizo. Hawa husema lolote linalokuja mdomoni. Shida inakuja anapotakiwa kwa mfano kuthibitisha alilosema. Wengi huishia kuomba radhi, lakini wapo ambao huendelea kushupaza shingo na kuendelea kuishi na uongo wao.

Mwaka 1996 mwanasiasa machachari wa upinzani nchini, Augustine Mrema, alipata kupasua ‘bomu’ lake kubwa katika mkutano wa hadhara wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo jimbo la Temeke, jijini Dar es Salaam. Mrema akiwania ubunge jimboni humo, alimtuhumu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) bila kumtaja, wakati huo alikuwa Rais Benjamin Mkapa, kuwa alihusika katika kashfa ya rushwa ya Sh. milioni 900. Tuhuma hizo zilimgharimu pakubwa Mrema. Kwanza iliundwa Kamati ya Bunge kuchunguza tuhuma hizo na ikathibitika zilikuwa za uongo. Kisha ikafunguliwa kesi ya jinai dhidi ya Mrema mahakamani kwa kulidanganya Bunge. Kilichomponya Mrema mahakamani ni kile cheti alichokuwa amepewa na Bunge baada ya kuhojiwa na kamati yake, kwamba kisheria mtu akishapewa cheti hicho hawezi tena kushitakiwa kokote. Hivyo kesi yake ikatupwa.

Hii ilikuwa ni kesi iliyovuta hisia za watu wengi, lakini la muhimu zaidi ilikuwa ni kipimo kwa wanasiasa kwamba wanapozungumza majukwaani ni kwa kiwango gani wanajiridhisha na yale wanayosema. Ingawa kesi hii haikufikisha mwisho hulka ya wanasiasa kusema lolote tu wawapo majukwaani, inaweza kuchukuliwa kama kipimo na msingi wa kutaka siasa ziendeshwe kwa kusema ukweli. Ni bahati mbaya bado hamu, kiu na shauku ya kutaka kusema lolote majukwaani ni ugonjwa ambao wanasiasa itawachukuwa karne nyingi kuacha.

Wiki iliyopita mkoani Shinyanga Katibu wa CCM wa Itikadi, Mafunzo na Uenezi, Amos Gabriel Makalla (53) naye amepasua ‘bomu’ lake. Hili lililipuka kwa kishindo kikubwa. Makalla alituhumu viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwamba wana mpango mbaya. Mpango huo ni wa kuingiza virusi vya ebola na mpox nchini ili kuwaambukiza Watanzania. Watanzania wakishaambukizwa virusi hivyo, itakuwa vigumu kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Makalla alituhumu kwamba Chadema wanaendesha kampeni ya kuchangisha fedha ‘matone matone’ ili kufanikisha kupata fedha za kununua virusi hivyo. Nia yao ni kutekeleza mpango wao wa ‘No Reforms, No Election’ yaani kama hakuna mabadiliko ya kisheria, hakuna uchaguzi.

Ingelikuwa maneno haya yamesemwa na mtu mdogo kisiasa, wala isingelikuwa ni jambo la kusumbua akili za watu. Makalla siyo mtu wa mtaani. Ni kiongozi. Anasimamia idara muhimu na nyeti ya Chama tawala. Ndiye mtu anayetumwa kuwasilisha ujumbe kwa umma baada ya vikao vya juu kabisa vizito vya chama hicho kukutana. Kiti alichokalia Makalla pale makao makuu ya CCM siyo kiti kidogo. Ni sehemu ya sekretarieti ya CCM. Ni mjumbe wa vikao vyote vikubwa vya CCM. Kuanzia Mkutano Mkuu, Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho. Kwa lugha ya mtaani Makalla ni miongoni mwa vigogo wa CCM kwa maana ya kiti alichokalia.

Kwa bahati mbaya kwamba tangu Makalla ametoa tuhuma hizo umma haujasikia kokote vyombo vya ulinzi na usalama vikichukuwa hatua za kushughulikia jambo hili. Kama wanafanya lolote, basi ni  kimyakimya. Hakuna kauli siyo ya Jeshi la Polisi, siyo ya Wizara ya Afya yenye wajibu wa kulinda afya za Watanzania wote, wala Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, yenye wajibu wa kulinda na kusimamia nidhamu ya vyama vya siasa ili visije kuleta taharuki kwa umma na kufanya watu waishi kwa hofu.

Katika hali ya kawaida kabisa kauli ya Makalla kwamba kuna chama cha siasa kinapanga kuingiza virusi hatari vya ebola na mpox nchini, ni mbiu imepigwa. Ni yowe imepigwa ya kutaka kulihami taifa dhidi ya hujuma kubwa na nzito za kutaka kuwaangamiza Watanzania. Ni kauli ya kuutaka umma ujihami dhidi ya njama hizo kwa kuwa virusi vya magonjwa aliyotaja Makalla hayana tiba wala chanjo. Ni magonjwa ambayo kwa sasa hivi wanasayansi kote duniani wanakuna vichwa kutafuta tiba na chanjo dhidi yake.

Lakini la muhimu zaidi, dunia imekwisha kukubaliana miaka mingi iliyopita kwamba matumizi ya silaha za kibaolojia dhidi ya binadamu ni kosa kubwa. Ni uhalifu wa kivita. Haya ni makosa ambayo jumuiya ya kimataifa kwa pamoja wamekubaliana kwamba hayawezi kuvumiliwa, haijalishi ukubwa wa nchi na uwezo wa tekinolojia, matumizi ya silaha za kibaolojia dhidi ya binadamu ni uhalifu usiovumilika.

Sasa tujiulize, Makalla kama kiongozi, kama mtu mzima, ikiwa kweli alikuwa na taarifa nyeti kama hizi, sehemu ya kuzimwaga ni kwenye mkutano wa hadhara? Ili wale wananchi wafanye nini? Wana uwezo wa kuwahoji au kuwakamata viongozi wa Chadema? Wana uwezo wa kuwafunguliwa mashitaka? Wana uwezo wa kuanzisha uchunguzi huru kubaini ukweli wa jambo hili? Kwa nini Makalla akaenda kupasua ‘bomu’ hilo sehemu kama ile, alikusudia kupata nini?

Makalla siyo mgeni wa madaraka na kukalia nafasi kubwa na nyeti. Makala alipata kuwa mbunge wa Mvomero kati ya mwaka 2010 hadi 2015. Ni katika kipindi hicho aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuanzia mwaka 2012 hadi 2014, na baadaye Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji mwaka 2015. Makalla amepata kuwa Mkuu wa Mkoa katika mikoa ya Kilimanjaro, Mbeya, Katavi na Dar es Salaam.

Nafasi zote hizo zilimpa fursa ya kuifahamu serikali inavyofanya kazi, kwa maana hiyo hakuna njia asiyoijua ya kuwasilisha taarifa nyeti kwa wahusika na katika mazingira ambayo hayataamsha taharuki kubwa kwa umma. Je, Makalla alisahau kuwa kuna njia hizo?

Kwa watu makini wanaojali na kuheshimu nafasi walizokabidhiwa katika ofisi za umma, madai ya Makalla juu ya virusi vya elola na mpox kuingizwa nchini ili kuwaambukiza watu kwa makusudi, siyo ya kuchukuliwa kwa wepesi hata kidogo. Hapo juu nimekumbushia kesi aliyokumbana nayo Mrema kwa kuzusha tu jukwaani kwamba Rais Mkapa alikuwa amehusika katika kashfa ya milioni 900, ili kuonyesha kuwa kuna kuwajibika kwa maneno mazito yanayosemwa hadharani, tena yanapokuwa yanatoka kwenye vinywa vya viongozi waliokalia ofisi za umma.

Ni hakika kama suala hili litapita tu kama vile kufagia uchafu na kuufunika kwenye zulia, tujue tu tunazidi kufanya mfumo wa uendeshaji wa siasa zetu kama taifa kukosa staha na uwajibikaji. Ipo hatari kubwa sana ya kuruhusu viongozi wetu waseme lolote tu linalokuja kinywani. Hatari hii ni kuzidi kuimarisha dhana potofu kwamba kusema uongo ni sehemu ya kuendesha ofisi za umma. Ni matarajio ya wengi kwamba jambo hili la watu kwenda kununua virusi halitaachwa tu lipite hivi hivi bila ukweli kujulikana. Tutafakari.

spot_img

Latest articles

SERIKALI ITAENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI-MAJALIWA

Na Mwandishi Wetu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kufanya maboresho zaidi ya mazingira...

ALLY KAMWE  AKAMATWA NA POLISI AACHIWA  KWA DHAMANA

Na Mwandishi Wetu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, SACP Richard Abwao amesema Jeshi la...

Bado watu wanapotea, yu wapi wa kuzuia hali hii?

ASKOFU wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dk. Benson...

Dkt. Biteko ashiriki uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Pwani

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko leo Aprili 2, 2025...

More like this

SERIKALI ITAENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI-MAJALIWA

Na Mwandishi Wetu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kufanya maboresho zaidi ya mazingira...

ALLY KAMWE  AKAMATWA NA POLISI AACHIWA  KWA DHAMANA

Na Mwandishi Wetu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, SACP Richard Abwao amesema Jeshi la...

Bado watu wanapotea, yu wapi wa kuzuia hali hii?

ASKOFU wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dk. Benson...