Serikali inafanyia kazi maboresho ya tozo kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI kupitia Wizara ya Madini inaendelea na juhudi za kupunguza mzigo wa tozo kwa Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu hapa nchini kwa kufanya mapitio ya ada na ushuru mbalimbali unaotozwa katika mnyororo wa uchimbaji na uchenjuaji wa madini hayo.

Hatua hiyo imebainishwa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, leo Februari 7, 2025, Bungeni Jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Busanda, Tumaini Magessa ambaye alitaka kujua ni lini Serikali itapitia upya tozo zilizopo kwenye mnyororo wa uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu zinazowaelemea Wachimbaji Wadogo.

Katika majibu yake, Waziri Mavunde amesema kuwa kupitia Mkakati wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI), Wizara ya Madini imefanya utafiti wa tozo 66 zinazotozwa na Halmashauri mbalimbali katika shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu na kutaja baadhi ya tozo hizo kuwa ni ushuru wa karasha, ada ya ukaguzi, kodi ya ongezeko la thamani (VAT in leaching/CIP), ushuru wa kusafirisha miamba ya madini, na visusi (mabaki ya miamba baada ya uchenjuaji).

“Katika kutatua changamoto hizi, Wizara iliitisha kikao Mwezi Agosti, 2024 Mkoani Singida ambacho kilishirikisha Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Wizara ya Fedha, Tume ya Madini, STAMICO, Halmashauri za Wilaya (Ikungi, Chunya, Kahama, Msalala, Meatu, Shinyanga, Mtama na Lindi), FEMATA na TAWOMA. Rasimu ya Mapendekezo ya Maboresho tayari imeshaandaliwa na ipo katika hatua ya kufanyiwa mapitio na tathmini, ambapo Matokeo ya tathmini hiyo yatatusaidia katika kupanga tozo rafiki kwa wachimbaji wadogo,” amesema Mavunde.

Aidha, Waziri Mavunde ameongeza kuwa, Serikali inaendelea na maboresho makubwa ya mfumo wa kodi kupitia Tume ya Maboresho ya Kodi iliyoanzishwa na Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kwamba tume hiyo inatarajiwa kutoa mapendekezo yatakayosaidia kupunguza changamoto za kikodi zinazowakabili Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu na Sekta ya Madini kwa ujumla.

Hatua hizo zinadhihirisha dhamira ya Serikali katika kuboresha mazingira ya uchimbaji mdogo wa madini na kukuza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi.

spot_img

Latest articles

Dube awapa raha wananchi

Na Winfrida Mtoi BAO pekee lililofungwa na Prince Dube dakika ya 58, limeipa Yanga alama...

Mexico yatwaa taji la Miss Universe 2025, Ivory Coast namba tano

Na Mwandishi Wetu Mexico imeibuka mshindi wa taji la Miss Universe 2025 kupitia mrembo wake...

Kocha Yanga ataja mbinu kuingamiza FAR Rabat

Na Mwandishi Wetu KOCHA Mkuu wa Yanga, Pedro Concalves amesema falsafa yake katika mechi ya...

Zawadi za PIKU zafungua milango ya ujasiriamali kwa Watanzania

Na Mwandishi Wetu KATIKA kudhihirisha kuwa teknolojia inabadilisha maisha ya Watanzania, Jukwaa la Kidijitali...

More like this

Dube awapa raha wananchi

Na Winfrida Mtoi BAO pekee lililofungwa na Prince Dube dakika ya 58, limeipa Yanga alama...

Mexico yatwaa taji la Miss Universe 2025, Ivory Coast namba tano

Na Mwandishi Wetu Mexico imeibuka mshindi wa taji la Miss Universe 2025 kupitia mrembo wake...

Kocha Yanga ataja mbinu kuingamiza FAR Rabat

Na Mwandishi Wetu KOCHA Mkuu wa Yanga, Pedro Concalves amesema falsafa yake katika mechi ya...