Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limetoa ratiba ya shughuli kuelekea mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni mkoani Dar es salaam na Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani WHO Kanda ya Afrika Dkt Faustine Ndugulile.
Dkt. Ndugulile alifariki dunia usiku wa kuamkia Novemba 27, 2024 nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na ofisi ya Bunge, mwili wa marehemu Dkt. Ndugulie utawasili uwanja wa ndege wa Dar es salaam na kupokelewa na viongozi mbalimbali wa serikali na wawakilishi wa chama siku ya Ijumaa Novemba 29, 2024 majira ya saa 6:35 mchana na kupelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali ya JWTZ Lugalo.
Novemba 30, 2024 shughuli za maombolezo zitaendelea nyumbani kwa marehemu mpaka Disemba 1, 2024 saa 3:00 asubuhi ambapo mwili utakuwa umewasili nyumbani kwake Kigamboni jijini Dar es salaam kwaajili ya taratibu nyingine.
Saa 3:30 mpaka saa 8:00 mchana mwili utapelekwa viwanja vya Machava na kutoa fursa kwa wananchi kutoa heshima za mwisho kisha kurejeshwa nyumbani.
Siku ya Disemba 2, 2024 mwili wa marehemu utawasili viwanja vya Karimjee saa 3:10 na kufanyiwa Misa Takatifu, kutaja wasifu kisha salamu za pole na shukrani kutoka kwa familia.
6:30 mpaka 8:00 Mchana Mheshimiwa Rais atawaongoza Viongozi na Wageni mbalimbali kutoa heshima za mwisho na saa 8:00 – 9:00 alasiri msafara wa mwili wa Marehemu utaanza kuondoka Viwanja vya Karimjee kuelekea Makaburi ya Mwongozo Kigamboni kwaajili ya mazishi.
Dkt. Ndugulile alifanya kazi katika nyanja mbalimbali za tiba, afya ya umma na siasa ambapo mwanzo alianza kama daktari wa afya ya umma na kupanda kwenye nafasi za uongozi.
Alifanya kazi kama Msaidizi Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi katika Wizara ya Afya, ambapo aliongoza juhudi za kuboresha huduma za damu na uchunguzi wa magonjwa, na kuwa na mchango mkubwa katika programu za afya za kitaifa.
Katika ngazi ya kimataifa, alifanya kazi kama Mshauri Mkazi nchini Afrika Kusini, akichangia katika usimamizi wa mifumo ya afya ya kanda na mipango ya kukabiliana na magonjwa ya milipuko.
Alianza siasa mwaka 2010 alipochaguliwa kuwa Mbunge wa Kigamboni nafasi aliyoitumikia mpaka mauti ilipomkuta.
Dkt. Ndugulile aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Rais wa awamu ya tano, hayati Dkt. John Magufuli, Oktoba 2017.
Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2020, tarehe 5 Desemba 2020, katika Baraza la Mawaziri, aliteuliwa kuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Agosti 2024, Dkt. Ndugulile aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani WHO.
Uteuzi wake kama Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika ulikuwa ni mafanikio makubwa kwa Tanzania na bara la Afrika.
Dkt. Ndugulile amefariki akiwa na umri wa miaka 55 na alikuwa anatarajiwa kuanza rasmi jukumu lake WHO mnamo 2025.