
MWANDISHI WETU, DODOMA
TANZANIA imevuna dola za Marekani Bilioni 2.32 zaidi ya Sh. Trilioni sita za kitanzania kutokana na mauzo ya tani milioni 1.57 za mazao ya matunda na jamii ya kunde huko China, India, Marekani, Pakistan na Brazil.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema leo jijini Dodoma kuwa Serikali pia imewezesha upatikanaji wa soko la vanilla, pilipili manga, karafuu, nanasi, kakao, viazi mviringo, tumbaku na ndizi katika nchi hizo pamoja na Afrika Kusini ambayo yatafunguliwa siku chache zijazo.
Akizunguza kwenye ufunguzi wa Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Sherehe za Nanenane ya Mwaka 2024 katika viwanja vya Nzuguni, Majaliwa ametaja masoko mengine yaliyopatika kuwa ni kwa ajili ya nafaka hususan mahindi.
Amesema Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NRFA) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) imeingia makubaliano ya kuuza tani milioni 1.25 za mahindi.
“Kati ya hizo, tani 650,000 zitauzwa Zambia; tani 500,000 zitauzwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na tani 100,000 kwa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP),”anasema Majaliwa na kuongeza:
“Kwa upande wa wafugaji, hadi Aprili, 2024 jumla ya tani 13,745 za nyama zenye thamani ya dola za Marekani milioni 56zimeuzwa.” Ametaja nchi ambazo ni soko la bidhaa hizo kuwa ni Bahrain, Comoro, Hong Kong, Jordan, Kenya, Kuwait, Oman, Qatar, Rwanda, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Vietnam.
Amesema pia vipande 1,542,916 vya ngozi vyenye thamani ya shilingi bilioni saba vimeuzwa katika nchi za Nigeria, Togo, Kenya, Ethiopia na Pakistan.
Kuhusu sekta ya uvuvi, Waziri Mkuu amesema hadi kufikia Aprili, 2024, tani 41,271 za mazao ya uvuvi na samaki hai wa mapambo 134,572, wenye thamani ya sh. bilioni 515.78, waliuzwa katika nchi za Umoja wa Nchi za Ulaya, Canada, Marekani, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, China, Zambia, Uganda na Malawi.
Akielezea jitihada ambazozimechukuliwa na Serikali kuendeleza sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, Waziri Mkuu amesema sambamba na utashi na maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,Serikali imeendelea kuongeza ajira kwa vijana na wanawake kupitia programu ya Jenga Kesho Iliyo bora (BBT).
“Kupitia programu hiyo, vijana 686 wanaendelea na kilimo biashara katika mashamba ya pamoja na tayari wameanza uzalishaji. Kwa upande wa mifugo, vijana 161 wanaendelea na programu ya unenepeshaji wa ng’ombe katika vitalu vya Ranchi za Taifa (NARCO). Sekta ya uvuvi nayo haikuachwa nyuma tayari vijana 200 wamehitimu mafunzo na vijana 300wanaendelea na mafunzo ya ukuzaji wa viumbemaji,” anasema.
Mapema Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema wizara yake imeanza kutekeleza maagizo ya Rais Samia ya kujenga miundombinu ya kudumu kwenye viwanja vya kanda yanakofanyika maonesho ya NaneNane ili kuwezesha maeneo hayo kufanya kazi mwaka mzima.
Alisema uwanja wa Nzuguni ambao unahudumia mikoa ya Dodoma na Singida, utajengwa kwa awamu tatu hadi kukamilika kwake na utagharimu sh. bilioni 40. “Tumeanza kujenga uzio, kutakuwa na maeneo shughuli za uzalishaji kwa mwaka mzima, kutakuwa na kumbi za mikutano na incubation centers (vituo atamizi) kwa ajili ya vijana wanaofanya shughuli za teknolojia,”anasema.
Amevitaja viwanja vingine vitakavyoboreshwa kuwa ni vya Johh Mwakangale (Mbeya), Julius Nyerere (Morogoro), Themi (Arusha) na Ngongo (Lindi). Alisema katika mwaka ujao wa fedha 2025/26 vitaanza kujengwa viwanja vya kanda za Magharibi na Ziwa.
Amesema kwenye kilele cha maadhimisho hayo Agosti 8, mwaka huu, Rais Dkt. Samia anatarajiwa kuzindua kiwanda cha kuunganisha matrekta kinachojengwa hapohapo Nzunguni na vifaa kwa ajili ya wakulima. Atazindua matrekta 500 na powertiller 800 za kwanza.
Amesema lengo ni kuzalisha matrekta 10,000 ifikapo mwaka 2030 ili wakulima wadogo waweze kukodi. “Mkulima hana haja ya kununua trekta kwa shilingi milioni 60, anahitaji shamba lake lilimwe kwa trekta, lipigwe harrow, lipandwe kwa planter, apate boom sprayer. Serikali inawekeza fedha kwenye eneo hilo,” amesema.
Naye, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti amesema kwa siku nane za maonesho hayo, washiriki watashuhudia mashindano ya mifugo ili kila mfugaji aone kuwa matumizi ya teknolojia ya mifugo yanawezekana kufanyika katika maeneo yao.