Matusi mitandaoni hayatanizuia kufanya mageuzi ya kiuchumi-Rais Samia

Na Mwandishi Wetu, Media Brains

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema anafahamu kuhusu matusi yanayoendelea katika mitandao ya kijamii, lakini ameamua kukaa kimya kwani lengo lake kuu ni kufanya mageuzi ya kiuchumi nchini.

Rais Samia alibainisha hayo Juni 11, 2024, wakati wa hafla ya kukabidhi gawio kwa serikali kutoka mashirika ya umma na binafsi iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam. Hafla hiyo ilikuwa na kauli mbiu: “Mageuzi ya Mashirika ya Umma na Wajibu wa Kuchangia Maendeleo ya Tanzania.”

“Najua kuna matusi mengi ninayotukanwa, lakini najigeuza kuwa kama chura kiziwi ambaye hayasikii. Lengo langu ni kuleta mageuzi ya kiuchumi ndani ya nchi yetu ili maendeleo yapatikane,” alisema Rais Samia.

Rais Samia alieleza hadithi ya chura aliyeshinda shindano kwa kupanda juu licha ya kelele nyingi za kujaribu kumvunja moyo. Chura huyo hakuweza kusikia kelele hizo na aliendelea mpaka akafanikiwa. Alijifananisha na chura huyo kwa kusema, “Mimi kazi mliyonipa nasimama na kuifanya. Matusi ninayotukanwa, na kelele ninazopigiwa, hazitanizuia kutimiza malengo yangu.”

Aliongeza kuwa, “Yeyote anayetaka kunikera, anikanyagie uchumi wangu. Katika mageuzi haya, tutakanyaga wengi ambao hawataki kwenda mbele na ndio watakaopiga kelele nyingi sana. Mliopo kwenye mashirika ambao hamtaki kukanyagiwa, nendeni mkafanye kazi ili kuleta maendeleo,” alisema Rais Samia.

Akizungumzia kuhusu bandari, Rais Samia aliipongeza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa kutoa gawio la shilingi bilioni 153.9 kwa serikali. Alisema wale wanaopinga mageuzi hayo hawajui faida zake, na anaamini TPA itaendelea kutoa gawio kubwa zaidi kwa serikali kutokana na mageuzi yaliyofanyika.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alisema serikali inakamilisha mchakato wa kuandikisha mashirika ya umma kwenye soko la hisa ili wananchi wanunue hisa na kuwa wamiliki wa mashirika hayo. Pia, alieleza kuwa serikali ipo katika hatua za mwisho za kufuta au kuunganisha mashirika yasiyofanya vizuri.

Awali, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, alitoa taarifa ya kupokea gawio na michango kutoka kwa mashirika na taasisi. Alisema hadi sasa wametoa gawio la shilingi bilioni 637, na wanatarajia kufikia shilingi bilioni 850 kufikia mwisho wa mwaka huu. Pia, alisisitiza umuhimu wa ubunifu na kuongeza mapato ya taasisi ili kuchangia mfuko mkuu wa serikali na kusaidia maendeleo ya taifa.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Jenerali Mstaafu Venance Mabeyo, alisema bodi za mashirika ya umma zina wajibu wa kulinda maslahi ya umma kwa kusimamia utendaji kazi na kuongeza ukusanyaji wa mapato.

Hafla hiyo ilihitimishwa kwa kusisitiza umuhimu wa mashirika ya umma na taasisi kuendelea kuchangia uchumi wa taifa na kupunguza mzigo kwa serikali. Rais Samia alisisitiza kuwa mageuzi haya ni kwa manufaa ya wote, na wale wanaopinga hawataweza kuzima azma yake ya kuleta maendeleo nchini.

spot_img

Latest articles

Simbu ang’ara tena Boston Marathon, ashika nafasi ya pili

Na Mwandishi Wetu Mwanariadha nyota wa Tanzania, Sajinitaji Alphonce Simbu, ameendelea kufanya vizuri Boston Marathon...

Tanzania mwenyeji Miss World 2027, Serikali yajipanga kuandika historia mpya duniani

Na Winfrida Mtoi TANZANIA imethibishwa rasmi kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa la urembo duniani ‘Miss...

Latra yatangaza nauli mpya za mabasi, daladala

Na Mwandishi Wetu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetoa bei mpya za nauli kwa...

Serikali yatoa neno vipaji vya kuogelea Afrika Mashariki vikichanua Dar

Na Winfrida Mtoi ​MASHINDANO ya kuogelea kwa watoto ya ‘East Africa Development Swimming Gala’ yameanza...

More like this

Simbu ang’ara tena Boston Marathon, ashika nafasi ya pili

Na Mwandishi Wetu Mwanariadha nyota wa Tanzania, Sajinitaji Alphonce Simbu, ameendelea kufanya vizuri Boston Marathon...

Tanzania mwenyeji Miss World 2027, Serikali yajipanga kuandika historia mpya duniani

Na Winfrida Mtoi TANZANIA imethibishwa rasmi kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa la urembo duniani ‘Miss...

Latra yatangaza nauli mpya za mabasi, daladala

Na Mwandishi Wetu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetoa bei mpya za nauli kwa...