Anahitajika wa kuchutama ulaghai Ngorongoro

KATIKA kipindi cha wiki mbili suala la uhamishaji wa wananchi wanaoishi Ngorongoro limetawala vichwa vya habari, mijadala katika mitandao ya kijamii na hata kwenye vijiwe vya kahawa. Ni habari ya moto.

Moto wa mjadala huu umekolezwa na mambo mawili makubwa. Mosi, uamuzi wa watu jamii ya Wamasai kuandamana na kupiga kambi uwandani usiku na mchana kwa siku kadhaa wakitaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, akazungumze nao ili kusikiliza kilio chao, kwani walikuwa wanahamishwa kwenye ardhi yao pasi na ridhaa yao.

Pili, tangazo la serikali namba 673 (Amri ya Marekebisho ya Amri ya Mgawanyo wa Maeneo ya Utawala katika serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) ya Agosti 2, 2024, ambayo ilifuta vijiji na vitongoji kadhaa wilayani Ngorongoro, nayo iliongeza uzito na kuthibitisha kile ambacho kwa muda sasa kimekuwa ni hofu ya wakazi wa wilaya hiyo kwamba kulikuwa na njama za kutaka kuwahamisha kwa nguvu kutoka katika ardhi yao.

Mlolongo huu wa mambo pia ulijionyesha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ambalo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, imedaiwa kuhamisha majina ya wakazi wa Ngorongoro kwenda Msomera, Handeni, bila ridhaa yao. Tangu mwaka 2021/22 kumekuwa na juhudi za chini kwa chini za kulazimisha jamii inayoishi Ngorongoro kuhama maeneo hayo kwa hila.

Kwa mfano, serikali ilihamisha fedha za huduma ya jamii -elimu na afya- kutoka Halmashauri ya Ngorongoro kwenda Handeni. Hatua hizi zote zilichukuliwa ili kudidimiza huduma hizo wilayani Ngorongoro, hivyo kufanya maisha ya wakazi wake kuwa magumu. Nia ikiwa ni kuwalazimisha kuondoka katika maeneo hayo.

Serikali imekuwa ikiimba kwa kitambo sasa kwamba wakazi wa Ngorongoro wanaohama kwa hiari, wanapata maisha bora katika wilaya ya Handeni. Picha za nyumba bora, mashamba yaliyostawi na hata shule vimekuwa ni vielelezo vya hali ya maisha mapya kwa wale walioondoka Ngorongoro kwenda Msomera, Handeni. Kampeni hizi zimekuwa zikipigiwa chapuo na watu maalum kwa kutumia vyombo maalum vya habari.

Eneo la Ngorongoro kwa kitambo sasa limekuwa ni kama uwanja wa vita ambako siyo rahisi kwa raia wa kawaida kufika achilia mbali waandishi huru wa habari.

Kama ambavyo wahenga walitufundisha kwamba mbaazi zikishindwa kuzaa/kustawi, husingizia jua, ndivyo kumekuwa na visingizio dhidi ya hatua ya jamii inayoishi Ngorongoro kuandamana na kuamua kukesha wakitaka Rais akaonane nao. Visingizio hivi kama ambavyo imekuwa ada, vimeelekezwa dhidi ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) ambayo yanafanya kazi wilayani humo kwa upande mmoja, na majirani wa Tanzania, Kenya kwa upande mwingine. Kwamba kuna watu wa jamii ya Kimasai kutoka Kenya ndiyo wanahamasisha upinzani wote wa watu kuhamishwa kutoka katika ardhi yao ambayo ni urithi kutoka kwa mababu na mababu zao.

Baada ya mambo kuwa magumu, ghafla likafunguliwa shauri mahakama kuu Arusha ambalo lilifanikiwa kuzuia Tangazo la Serikali la kufuta vijiji na vitongoji hivyo. Kwa mwendo na kasi ya mwanga, mawaziri wawili, William Lukuvi (Sera, Uratibu na Bunge) na Profesa Paramagamba Kabudi (Sheria na Katiba) wakatua Ngorongoro kuwafikishia ujumbe wananchi waliokuwa wamekesha na kushinda uwandani kwa siku kadhaa kwenye baridi kali, kwamba Rais Samia amesikia kilio chao. Kwamba amesimamisha ufutaji wa vijiji na vitongoji katika eneo hilo. Aidha, mawaziri hao walisema kuwa Rais pia ameamuru huduma za kijamii zilizokuwa zimesitishwa wilayani Ngorongoro zirejeshwe. La mwisho, kwamba Rais anapanga kuonana ana kwa ana na wakazi wa Ngorongoro mahali patakapoelezwa baadaye ili kusilikiza malalamiko yao.

Ukiwasikiliza mawaziri hawa, unaweza kudhani kwamba uamuzi wa kuwaondoa wakazi wa Ngorongoro katika ardhi yao, uamuzi wa kufuta vijiji na uamuzi wa kuwapoka haki yao ya kupiga kura katika maeneo ambayo wamekuwa wanaishi miaka yote hii, haukutokana na serikali. Ni kama serikali imeenda Ngorongoro kuzima tatizo ambalo lilisababishwa na mamlaka nyingine. Yaani serikali hata katika uamuzi wa kasi ya mwanga kwenda Ngorongoro na kukutana na wananchi hao, haionyeshi kukiri kwamba ndiyo chanzo cha kadhia yote ya Ngorongoro. Haionyeshi kutambua kuwa imewaonea na kuwadhalilisha mno wakazi wa Ngorongoro.

Kadhia ya Ngorongoro imejisimika katika hoja kuu mbili. Moja, ongezeko kubwa la watu ambao wanatishia uhai na uhimilivu wa uhifadhi katika Eneo la Mamlaka ya Ngorongoro. Mbili, ongezeko kubwa la mifugo ambayo pia imekuwa tishio kwa ustawi wa uhifadhi. Kwa maana hiyo, hali hiyo inalazimisha hatua kuchukuliwa ili kunusuru uhifadhi. Ni jambo linalofikirisha na linalostahili hatua shirikishi za kuokoa Ngorongoro, lakini zenye sura inayozingatia haki za binadamu.

Wakati kukiwa na hoja hizi, utaratibu uliotumika kufikiwa kwa lengo kuu la kufanya uhifadhi Ngorongoro kuwa endelevu, hauonyeshi kutambua kuwapo kwa makandokando mengine katika kufikiwa kwa uendelevu huo. Kwa mfano, kuna taarifa kwamba kumekuwa na ujenzi wa viwango vya juu wa hoteli za kitalii mbugani, uwepo wa misafara mingi ya magari ya utalii ambayo pengine, mazingira ya sasa ya Ngorongoro hayahimili shughuli hizi. Kuna suala la kuibuka kwa uoto ambao siyo asilia katika eneo la Ngorongoro yakiwamo magugu ambayo yanaathiri malisho ya wanyama pori. Kwa kifupi, uhifadhi Ngorongoro unakabiliwa na changamoto nyingi. Kwa kiwango kikubwa chimbuko lake ama ni sera au maamuzi ambayo siyo sahihi sana katika uendelevu wa eneo hilo.

Kuna changamoto kubwa, serikali inaonekana kama imejifungia ndani na kuibuka na mipango na maamuzi ya kutaka kuisaidia Ngorongoro, bila kushirikisha jamii ambayo kwa miaka na miaka, imekuwa ikiishi na wanyamapori kwa amani. Kimsingi jamii hiyo ni wahifadhi asilia. Utaratibu huu wa kutokutaka kuwasikiliza mpaka pale walipoamua kushinda na kukesha uwandani kwa siku kadhaa, umeonyesha udhaifu mkubwa sana kwa serikali.

Hali hii pia ndiyo imeshamiri Loliondo. Kwa miaka sasa kumekuwa na mvutano mkubwa. Wapo watu wamepoteza ardhi yao bila fidia. Wapo watu wamekimbia familia zao kwa hofu ya kusakwa na dola kwa makosa ambayo kimsingi yamechangiwa na serikali yenyewe.

Kwa mfano, mapema mwezi huu, shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International (AI) lilitoa ripoti ya kina juu ya hali ilivyo Loliondo. Ripoti hiyo iliyopewa jina la Tanzania: Business as usual in bloodied land? Role of businesses in forced evictions in Loliondo, Tanzania, inaeleza kwa kina nguvu za wenye mitaji wanavyosukuma ajenda yao ndani ya maamuzi mbalimbali ya serikali kuhusu uhifadhi. Ripoti hiyo inaeleza shughuli za kibinadamu zilivyotanda katika eneo la kilometa za mraba 1,500 ambazo watu waliondolewa kwa nguvu kisha kutangazwa Pori Tengefu la Pololeti. Uchunguzi wa AI unaonyesha shughuli nyingi za ujenzi wa majengo ya kudumu katika eneo hilo ambalo watu waliondoshwa kwa nguvu kwa kisingizio cha kusaidia uhifadhi wa shoroba baina ya Hifadhi ya Mbunga ya Taifa ya Serengeti na Mamlaka ya Eneo la Ngorongoro.

Jambo moja ambalo kwa sasa hivi liko wazi kuhusu suala la Ngorongoro ni mkorogano ndani ya serikali. Ni vigumu kuelewa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, anaweza vipi kutoa tangazo la serikali la kufuta vijiji na vitongoji bila ridhaa kupatikana ndani ya serikali? Au inawezekana vipi Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kufikia uamuzi wa kuhamisha wapigakura kutoka Ngorongoro kwenda Handeni kimyakimya bila kuwashirikisha wapigakura wanaohamishwa? Suala la Ngorongoro ni sawa kabisa na ile simulizi kwamba mtu anatengeneza tatizo aje kulitatua ili kutafuta imani ya wananchi, jambo ambalo ni la kilaghai kabisa. Katika suala la Ngorongoro serikali inapaswa kuchutama.

spot_img

Latest articles

Tulia alipoteza fursa ya kuokolewa uhai wa Kibao

INAWEZEKANA Agosti 27 2024 ilikuwa ni siku ambayo maisha ya Ally Mohamed Kibao yangeokolewa...

DCEA yakamata kilo 1,815 za skanka

Na Mwandishi Wetu Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewakamata...

Waziri Mkuu: Suala la mazingira liwe ajenda ya Kitaifa

Na Mwandishi Wetu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema suala la uhifadhi wa mazingira liwe...

NECTA yawaonya wamiliki na wakuu wa shule

Na Winfrida Mtoi Baraza la Mtihani la Tanzania (NECTA), limewataka wamiliki na wakuu wa shule...

More like this

Tulia alipoteza fursa ya kuokolewa uhai wa Kibao

INAWEZEKANA Agosti 27 2024 ilikuwa ni siku ambayo maisha ya Ally Mohamed Kibao yangeokolewa...

DCEA yakamata kilo 1,815 za skanka

Na Mwandishi Wetu Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewakamata...

Waziri Mkuu: Suala la mazingira liwe ajenda ya Kitaifa

Na Mwandishi Wetu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema suala la uhifadhi wa mazingira liwe...